BAADA ya kusota na kutaniwa kwa misimu minne mfululizo bila makombe, wanachama wa Simba mkoani Mwanza wamesema msimu ujao ni mwisho wa dhihaka zote na wanataka jambo moja tu, ambalo ni ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba imeendelea kuambulia patupu na kuwa mnyonge mbele ya mtani wake, Yanga ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho (FA).
Mashabiki na wanachama wa Simba katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema, wikiendi iliyopita walifanya sherehe kubwa ya Simba Day iliyounganisha matawi 42 wilayani humo na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuchangia damu katika kituo cha afya Kakobe.
Mwenyekiti wa matawi ya Simba Mwanza, Ashraf Mukadam alisema licha ya kuboresha kikosi chao kwa usajili wa maana, lakini mashabiki wasitegemee ushindi kupatikana kirahisi kwani wapinzani wao wamejiandaa kuwahujumu.
“Mechi zetu zitakuwa ni ngumu wengine hawachezi lakini wataikamia Simba, niyaombe matawi yote tushirikiane kuhakikisha tunaipa sapoti timu,” alisema Mukadam na kuongeza;
“Na mimi nina imani 2025/2026 Simba ni bingwa wa Ligi Kuu, hii ni ahadi natoa na Mwenyezi Mungu atatusaidia tutafanikisha.”
Mwenyekiti wa Simba Wilaya ya Buchosa, Juma Muheza alisema usajili uliofanywa na viongozi unakwenda kukomesha unyonge uliokuwepo kwa misimu minne na kukosa makombe.
“Usajili uliofanyika nafikiri ni wa kuogopwa, mwaka huu lazima kombe liingie nyumbani lilikozoea kukaa,” alisema Muheza.
Makamu Mwenyekiti wa Simba tawi la Kamanga Sokoni, Mariam Kapalama, alisema; “2025/2026 moto utawaka naomba wana Simba wote tuungane na tushirikiane tukawape sapoti wachezaji wetu.”
Baraka Bunyonga, Katibu wa tawi la Nyakalilo alisema hana shaka na timu yake kwani usajili uliofanyika unamfanya alale usingizi mnono, huku Msemaji wa tawi la Kasalaji, Joseph Lutema akitamba msimu ujao hawana kikwazo cha kuwanyima ubingwa wa Ligi Kuu.
Msemaji wa Simba Halmshauri ya Buchosa, Faustine Protus aliwataka mashabiki na wanachama kujipanga kwa msimu ujao kuiunga mkono timu yao kwa kununua jezi na kwenda viwanjani kuhakikisha inapata matokeo mazuri.
“Tumepitia misimu minne ya maumivu, tumehangaika sana kupata ushindi lakini tujipange kwa msimu huu kuhakikisha tunarudisha heshima yetu kama tulivyokuwa tumezoea misimu iliyopita,” alisema Protus.