Kigoma. Kikundi cha wanawake wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) cha Kiganamo kilichopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kimekuwa kikundi cha mfano kutokana na kuzidi kuimarika na kuongeza hamasa kwa kupata wanachama wapya.
Kikundi hicho kijulikanacho kama Peer Mothers kinatoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya kwa wajawazito na wanaonyonyesha huku elimu hiyo ikionekana kuleta matokeo mazuri kwa wahusika.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, idadi ya wanachama wa kikundi hicho imeongezeka kutoka wanane hadi wanachama 94 huku 18 kati yao wakiwa wajawazito na 76 wakiendelea na unyonyeshaji.
Hii inatokana na utayari wa wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wa kuwa na wenzao, huku dhima kuu ya kikundi hicho ikiwa ni utaoaji elimu na ushauri kuhusu kuzingatia taratibu na tahadhari dhidi ya VVU kwa wanawake wanaonyonyesha na wajawazito.
Kupitia umoja huo, watoto 37 waliozaliwa na kina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU katika kikundi hicho, hawana maambukizi, hali inayochochea mafanikio katika elimu ambayo wamekuwa wakipeana na kukutana na watalamu wa afya kila Jumatano.

Akizungumza baada ya kutembelewa na maofisa wa Shirika la Tanzania Health Program Suppoters (THPS), jana, Agosti 13, 2025, kinara muelimisha rika katika kikundi hicho, Gelesia Adriano amesema aligundulika kuwa ana maambukizi ya VVU mwaka 2007.
Amesema baada ya vipimo kuonyesha kuwa yeye na mume wake wameathirika, mtoto wao wa mwisho aliyekuwa na umri wa miezi 11, pia, alibainika kuwa ameathirika, hata hivyo alifariki dunia mwaka 2011 kutokana na kuchelewa kuanzishiwa matibabu.
Gelesia amesema licha ya kuanza dozi ya kufubaza virusi vya Ukimwi mwaka 2010, alikata tamaa ya maisha baada ya mume wake kufariki na hivyo kuamua kusitisha matumizi ya dozi kutokana na hali ya upweke aliyokuwa nayo.
Hata hivyo, amesema kupitia elimu aliyoipata baada ya kujiunga na kikundi chaa Kiganamo, amepata matumaini na ujasiri huku akisema kwa sasa anaishi kwa furaha na mume mwingine aliyempata huku wakiwa wamejaliwa kupata watoto watatu aliowazaa akiwa na VVU, lakini wao wakiwa hawajaambukizwa.
“Nawakaribisha wengine kujiunga kwenye kikundi, tunapeana elimu ya namna ya kumkinga mtoto na maambukizi. Pia, imetusaidia kuinuka kiuchumi kupitia wanachama ambao tuna vipato tofauti, tunafanya ujasiriamali kama kilimo cha bustani na kuelekezana kuhusu maisha,” amesema.
Naye Naomi Petro ambaye ameishi na maambukizi ya VVU kwa miaka tisa, amewahimiza wanawake wanaogundulika kuwa na maambukizi, kutoishi maisha ya hofu na badala yake wajiamini na kuwa karibu na jamii inayowazunguka kwa kushiriki shughuli za uzalishaji.
“Nilikuja kupima na kugundulika kuwa na maambukizi mwaka 2016, lakini sikukata tamaa na mpaka sasa nina watoto wanne na wawili niliwazaa nikiwa tayari nina maambukizi lakini wao hawana kwa kuwa nazingatia kanuni,” amesema.
Naomi ambaye kwa sasa ni mjamzito, amesema haoni sababu ya kuishi kwa hofu na msongo wa mawazo baada ya kujiunga katika kikundi cha uelimishaji cha Kiganamo ambacho kimemsaidia kuishi maisha ya kawaida bila woga huku akiwa huru kushiriki mambo ya kijamii.
Kwa upande wake, Consolata Amos amesema toka alipobainika kuwa na VVU mwaka 2007, amekuwa akiishi kwa furaha tofauti na wengine wanavyodhani huku akitoa wito kwa wanawake kutokata tamaa pindi wanapokutwa na VVU.
Licha ya kuwa na maambukizi, Consolata amebainisha kuwa anaishi maisha ya amani huku kwa sasa akiwa tayari anaishi na mume waliyeanzisha maisha ya ndoa na kwa sasa wamepata watoto wawili ambao wote hawana maambukizi ikiwa ni matokeo ya elimu ya kujikinga.
Mratibu wa VVU Wilaya ya Kasulu ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kiganamo, Dk Moshi Kigwinya amebainisha kuwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kupitia kikundi hicho.
Amesema kikundi hicho kimewarahisishia ufuatiliaji kwa wale wenye maambukizi mapya na kuifanya Wilaya ya Kasulu kuwa ya kwanza mkoani Kigoma kwa kufanya vizuri katika kudhibiti maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Ameongeza kwamba kutokana na mafanikio hayo, maambukizi katika wilaya hiyo yameshuka kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 1.0.
Msimamizi wa Shirika la THPS Mkoa wa Kigoma, Geofrey Tarimo amebainisha kuwa kupitia ushirikiano uliopo kati ya Serikali na taasisi binafsi, utekelezaji wa afua za kiafya ikiwemo udhibiti wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, umefanikiwa.
Amesema chini ya mradi wa Afya Hatua, shirika hilo limefadhili pikipiki, magari na watalamu wa afya ili kuwafikia wanaoishi katika maeneo ya vijijini kupitia vikundi hivyo vijulikanavyo kama Psycho-Socio Support Group (PSG).
Aidha, Serikali kupitia ushirikiano na Shirika la THPS kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na CDC, imekuwa ikitekeleza mradi wa Afya Hatua katika vituo 74 kwenye halmashauri za mkoa huo ikiwa na lengo la kudhibiti na kupunguza maambukizi ya VVU.
“Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2023/2024 na Tanzania HIV Impact Survey (THIS), mkoa huu una asilimia 1.7 na kuwa mkoa wenye maambukizi madogo zaidi Tanzania Bara,” amesema.