BAADA ya kumaliza kambi ya wiki mbili Karatu mkoani Arusha, kikosi cha Azam FC kimeondoka nchini kwenda Rwanda ambako ndiko kinamalizia maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Azam FC itakuwa timu ya pili kutoka Tanzania Bara kutua nchini humo ambapo Yanga tayari ipo jijini Kigali na leo Ijumaa inacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports.
Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa Karatu walicheza mechi mbili za kirafiki za ndani ambapo inaelezwa kwamba zilikuwa sehemu za maandalizi kwa vitendo dhidi ya kombaini ya Arusha na JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema: “Nafikiri huku (Rwanda) ndio tutaenda kucheza mechi za kirafiki za kiushindani na mpango ni kwenda kucheza mechi nne.”
Kikosi cha timu hiyo kilianza kambi mapema Julai 28 hadi 30 ambayo ilikuwa Chamazi jijini Dar es Salaam na baada ya hapo kikatimkia Karatu kuanzia Agosti Mosi hadi 14 kikifanya utalii wa ndani Mikumi na kurejea Dar es Salaam.
Awali, ilikuwa kikitoka Karatu mpango ulikuwa ni kwenda Afrika Kusini Agosti 15 hadi 30, lakini baada ya kubaini hakitaweza kupata mechi za kirafiki kimeamua kubadili nchi na kwenda Rwanda ambako kuna uhakika wa kupata michezo hiyo.