Arusha. Vitendo vya ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazokwamisha maendeleo ya nchi nyingi barani Afrika.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, kuna haja ya kujenga utamaduni wa uwajibikaji, uadilifu na uzalendo hasa miongoni mwa vijana.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alipokuwa akizungumza katika Jukwaa la Uwajibikaji kwa Vijana (YAIF) lililowakutanisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini, lililofanyika jijini Arusha.
Profesa Mkenda amesema kuwa ingawa matumizi mabaya ya rasilimali ni changamoto ya kidunia, nchi zinazoendelea kama za Afrika zina wajibu wa kipekee wa kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia athari, ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya bara hilo.
“Taifa linapaswa kulea kizazi cha viongozi vijana wenye maadili, wanaojali masilahi ya umma na watakaokuwa mstari wa mbele kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya wote. Huu ni msingi wa kuleta maendeleo endelevu barani Afrika,” amesema Profesa Mkenda.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kuanzia katika ngazi ya chini kwa kutoa elimu, kukuza uadilifu mashuleni na vyuoni, pamoja na kuwashirikisha vijana kama nguzo ya mabadiliko chanya katika jamii.
“Wakati mwingine linaweza kuvurugwa na mifumo, hivyo kusipokuwa na mipaka, kuangalia na kupiga kelele bara letu linaweza kurudi nyuma mno. Tufanye watu wafuatilie, wahoji lazima tujenge kama ni utamaduni na unaanza hapo ulipo usitarajie uanzie kwingine.
Profesa Mkenda amesema ndiyo maana somo la historia ya Tanzania na maadili linafundishwa mashuleni kwa lengo la kuwa wazalendo ili kulinda nchi na rasilimali zake.
“Nawasihi vijana ambao ndiyo viongozi wa kesho, tuwe na uwajibikaji katika kila mnalofanya kulinda na kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali zetu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu Ludovick Utouh, amesema klabu za vijana kutoka vyuo vikuu 11 hapa nchini, zimelenga kuongeza uelewa mpana wa uwajibikaji na utawala bora ikiwemo kuelewa madhara ya rushwa na mapambano dhidi yake, kabla ya kuingia kwenye soko la ajira au kujiajiri.
Utouh ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwajibikaji kwa umma ( Wajibu), amesema jukwaa hilo lilianzishwa kwa madhumuni ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora wenye uadilifu, uwajibikaji na uzalendo kupitia mafunzo mbalimbali.
Amesema jukumu la uwajibikaji wa umma katika rasilimali za umma ni la kila mmoja na Taifa linategemea mchango wa vijana katika hilo hasa kufuatia ongezeko lao nchini.
“Jukwaa hili hukutana mara moja kwa mwaka ambapo pamoja na masuala mengine wanajadili na kupanga mipango ya mwaka unaofuata, kuwajengea vijana dhana ya uwajibikaji, uzalendo na mapambano dhidi ya rushwa,” amesema.
Awali akisoma risala ya jukwaa la YAIF, Magreth Clement amesema jukwaa hilo limeandaliwa na Wajibu kwa lengo la kukuza na kuimarisha mazingira ya uwajibikaji wa fedha za umma na utawala bora nchini Tanzania.
Amesema wamefanikiwa kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo, taasisi na klabu za kupambana na rushwa na kushirikiana na viongozi wa serikali za wanafunzi kuimarisha uwazi wa mapato na matumizi ya fedha wanazokusanya.
Magreth ametaja mojawapo ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo kuwa ni ukosefu wa utambulisho rasmi wa kitaifa kwa klabu za uwajibikaji katika shule za msingi na sekondari.
Amesema hali hiyo inazikwamisha klabu hizo kupata ruhusa ya kuendesha midahalo, majadiliano na mafunzo katika shule husika, licha ya umuhimu wa shughuli hizo katika kujenga maadili na kuimarisha uwajibikaji kwa wanafunzi.
Mwakilishi wa walezi wa klabu ya wanafunzi kutoka vyuo 11 vya elimu ya juu nchini, Alphonce Kauki amesema walezi wameendelea kutumia nguvu na taaluma katika kuwalea vijana kwa kuzingatia kanuni, sheria na miongozo.