Uchaguzi wa TFF uko palepale, mahakama yajiweka kando

UCHAGUZI Mkuu wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), uliopangwa kufanyika kesho Jumamosi, Agosti 16, 2025, utafanyika kama ulivyopangwa baada ya kutupilia mbali shauri lililokuwa limefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine kuhoji uhalali wake.

Shauri hilo limetupiliwa mbali na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi,  leo Ijumaa Agosti 15, 2025,  baada ya kukubaliana na pingamizi lililowekwa na Wadhamini wa TFF, ambao walikuwa wajibu maombi wa pili, kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo

‎Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Agosti 16, 2025, mjini Tanga kwa ajili ya kupata rais wa shirikisho hilo inayowaniwa na rais anayemaliza muda wake, Wallace Karia, akiwa ni mgombea pekee, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

‎Hata hivyo, uchaguzi huo ulikuwa katika njiapanda kufanyika, kufuatia shauri hilo lililokuwa limefunguliwa na mawakili wanne,  Aloyce Komba, Jeremiah Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini.

Katika shauri hilo la maombi namba 19873/2025, ‎wajibu maombi walikuwa ni Baraza la Taifa la Michezo (BMT), lenye dhamana ya usimamizi wa michezo yote nchini ( mjibu maombi  wa kwanza), Wadhamini wa TFF (mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mjibu maombi wa tatu.

Waombaji katika shauri hilo walikuwa wanadai kuwa mchakato wa uchaguzi huo ni batili kwa kuwa unaoendeshwa chini ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za TFF, ambazo ni batili, kwani zinakiuka Sheria, Katiba ya Nchi na Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995.

‎Hivyo walikuwa  wanaiomba mahakama iridhie wafungue shauri la mapitio ya mahakama kuiomba itoe amri kuilazimisha  BMT kutekeleza wajibu wake wa kisheria katika kuisimamia TFF pamoja na mambo mengine, iielekeze TFF kufuta uchaguzi huo na kuanza upya.

‎Pia walikuwa wanaomba wakati wakisubiri uamuzi wa maombi yao hayo ya kibali cha kufungua shauri hilo la mapitio mahakama hiyo iridhie kutoa amri ya kudumisha hali ilivyo kabla ya siku ya uchaguzi, kusubiri shauri lao kusikilizwa pande zote.

Hata hivyo, ‎mjibu maombi wa pili, Wadhamini wa TFF waliibua pingamizi la awali wakiiomba mahakama isilisikilize shauri hilo, badala yake ilitupilie mbali, wakidai kuwa lina kasoro za kisheria zisizorekebishika, huku wakibainisha hoja 10.

Pingamizi hilo limesikilizwa leo, Ijumaa, Agosti 16, 2025. Kati ya hoja hizo 10, Mahakama imesikiliza hoja nne tu kwanza ambazo zilikuwa zinagusa mamlaka ya mahakama kusikiliza shauri hilo.

Katika uamuzi wake ambao umesomwa kwa niaba yake na Naibu Msajili Livin Lyakinana, Jaji Maghimbi amekubaliana na hoja za pingamizi hilo kuwa mahakama hiyo haina mamlaka.

Kama mawakili wa TFF walivyoieleza Mahakama, Jaji Maghimbi amesema kuwa kwa kuwa shauri hilo lilikuwa linalalamikia masuala ya ndani ya TFF na kwa kuwa TFF kwa mujibu wa Katiba yake ina vyombo vya kushughulikia migogoro baina yake basi mahakama inakosa mamlaka kushughulikia masuala hayo.

“Kwa hiyo ninakubaliana na pingamizi na shauri hili linatupiliwa mbali kwa gharama kwa mujibu maombi wa pili,” amesema Lyakinana.