Songea, Ruvuma – Agosti 15, 2025
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Wilaya ya Songea Raymond Aloyce, ameipongeza Shule ya Awali na Msingi Simagoo kwa mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, wakati wa mahafali ya nane ya elimu ya awali na ya nne kwa darasa la saba yaliyofanyika leo Agosti 15.
Akihutubia mgeni rasmi katika hafla hiyo, Aloyce alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu, wazazi na jamii kwa ujumla katika malezi na maendeleo ya mtoto.
Katika kuunga mkono jitihada hizo Aloyce aliahidi kuchangia vifaa vya michezo kwa shule hiyo ili kusaidia kuimarisha vipaji vya wanafunzi na kukuza nidhamu, afya na mshikamano wao kupitia michezo.
Aidha, alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora na salama, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na shule hiyo katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Shule ya Simagoo, iliyoanzishwa mwaka 2016 ikiwa na wanafunzi saba tu, sasa ina jumla ya wanafunzi 653 (wavulana 345 na wasichana 368). Mafanikio makubwa yamepatikana, ikiwa ni pamoja na ufaulu wa hali ya juu wa darasa la saba ambao umeiwezesha shule kushika nafasi ya pili kiwilaya, ya sita kimkoa, na ya 249 kitaifa.
Shule hiyo pia imefungua tawi jipya Peramiho, kuongeza idadi ya mabasi ya wanafunzi, na kuimarisha uwezo wa wanafunzi kusoma, kuandika na kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.
Hata hivyo changamoto bado zipo, Shule inakabiliwa na ucheleweshwaji wa ada, uhaba wa kompyuta, ukosefu wa ukumbi wa mikutano, mabwalo ya chakula, na vifaa vya michezo changamoto ambazo Aloyce aliahidi kushughulikia kwa kushirikiana na wadau wa elimu.
Wazazi waliohudhuria walieleza kuridhishwa na maendeleo ya watoto wao, wakibainisha kuwa Simagoo imewasaidia watoto wao kuimarika katika nidhamu, mawasiliano na stadi za maisha.