Hofu yazidi uokoaji ukiendelea mgodini Shinyanga, waliokolewa wafikia watano

Shinyanga. Hofu na wasiwasi vimezidi kuongezeka wakati shughuli za uokoaji zikiendelea kwenye mgodi wa wa Chapakazi wilayani Shinyanga, ili kuwapata mafundi 18 walionasa ardhini kwa siku ya tano.

Mwananchi lilishudia uopoaji wa miili ya walionasa katika mgodi huo shughuli iliyokuwa ikifanywa na vyombo vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi, huku viongozi wa Serikali ya Wilaya hiyo na Mkoa wakishuhudia kwa karibu.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amelieleza Mwananchi kuwa mpaka leo, Agosti 15, 2025 saa 10 na nusu jioni watu 7 kati ya 25 walikuwa wametolewa chini ya aradhi tangu kutokea kwa ajili hiyo, hata hivyo walioko hai ni watatu tu.

“Kati ya 25 mafundi saba wameokolewa, walioko hai ni watatu, kati yao wawili wameruhusiwa na tayari wameungana na ndugu zao, mmoja amepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando kwa kuwa alijeruhiwa kichwani.

Amesema uokoaji katika shimo moja umekamilika na amelifunga, baada ya watu wote sita waliokuwemo kuondolewa na katika mashimo mengine unaendelea.

“Duara namba 106 walikuwemo watu sita ambao wote wametolewa, watatu wako hai na watatu wamefariki. Mtu mwingine ametolewa kwenye duara namba 103 akiwa amefariki.

Amesema juhudi zinaendelea kuwatafuta 18 waliosalia, akieleza matumaini kwamba kulingana na urefu wa walipokuwa, upo uwezekano wa kuwapata wakiwa hao, kwa kuwa hewa inaingia, akikumbushia tukio la Nyangalata Novemba 2015, mkoani Shintyanga, ambako wachimbani waliokolewa baada ya siku 41.

Aidha, pamoja na juhudi zinazoendelea baadhi ya ndugu wa waliofukiwa mgodini wameiomba Serikali iongeze juhudi katika kuwatafuta ndugu zao, huku wakiwa wamejiandaa kwa matokeo yoyote.

Akizungumza na Mwananchi kwenye eneo la tukio, mkazi wa Kijiji cha Mwongozo Kata ya Mwenge Wilaya ya Shinyanga, Ernest Magese amesema amesema wasubiri matokeo yoyote lakini Serikali iongeze kasi, ili waweze kuwatoa ndugu.

“Leo ni siku ya tano, tunaomba Serikali watu wetu waweze kuwatoa haraka kwa hali yoyote, tuwapate ndugu zetu,” amesema Magese.

Naye Monica Andrea anasema “Nina kaka zangu wanne humu, tunakaa hapa, tunalala hapa tukimuomba Mungu ili waweze kuokolewa, tunaomba sana sana sana,” amesema.

Mkazi wa Misungwi, Mrisho Luneleja ameeleza, “nimekuja hapa kusubiri ndugu zetu ambao wako ardhini tunafanya juhudi za kuwatoa,” amesema Luneleja.

Naye Joseph Buzuka, amesema: “Nina vijana wangu wawili wako chini, tunasubiri hatima yao, wakati huu tumejiandaa kwa lolote kiakili, lakini tu wawatoe huko chini,” amesema.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 na kufukia watu 25 ambao walikuwa wakikarabati maduara ya mgodi huo.

Mkaguzi Mkuu wa kikundi cha Wachapakazi Gold Mine, Fikiri Mnwagi ambao ni wamiliki wa mgodi huo, alisema maduara hayo matatu yatiti wakati wa ukarabati na kufunika mafundi 25.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amefika eneo la tukio na kuzungumza na wananchi na wafanyakazi wa eneo hilo na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki  wa eneo hilo na kutoa shukrani kwa wakazi wa eneo hilo kwa juhudi za awali za uokoaji.