Kigoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amezindua kiwanda cha uzalishaji wa chumvi lishe (Cattle Lick) wilayani Uvinza, mkoani Kigoma.
Kiwanda hicho kimetajwa kuwa kitovu muhimu cha uchumi kwa Serikali, wananchi na wafugaji, hasa katika sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo, Agosti 15, 2025, Waziri Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Nyanza Salt Mine kwa kuanzisha uzalishaji wa chumvi lishe, hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya madini ya chumvi na kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo nchini.

“Chumvi ni moja ya virutubisho muhimu kwa mifugo, hususan kwa ng’ombe wanaonyonyesha, ndama na ng’ombe wenye mimba. Chumvi yenye madini ya Calcium na Phosphorus huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza uzalishaji wa maziwa, hamu ya kula kwa mifugo na unywaji wa maji,” amesema Waziri Mavunde.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza uagizaji wa chumvi lishe kutoka nje ya nchi, na hivyo kuokoa fedha za kigeni huku ukitoa ajira kwa wananchi wa Kigoma na maeneo jirani.
Kampuni ya Nyanza Salt Mine imeeleza kuwa ina mpango wa kuongeza uwekezaji wake hadi kufikia Sh20 bilioni ili kuimarisha uzalishaji na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
“Tunatamani kuona wananchi wakitumia rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa kutambua mahitaji ya soko, hivi sasa nchi yetu bado inaagiza chumvi lishe kwa ajili ya mifugo kutoka nje ya nchi.
“Hata hivyo, kupitia hatua hii ya kuanzisha uzalishaji wa chumvi lishe, tunatarajia kuwa katika miaka michache ijayo, Tanzania itaanza kujitengemea na hatimaye kuacha kabisa uagizaji wa chumvi lishe kutoka nje,” amesema Waziri Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde ameipongeza Kampuni ya Nyanza Salt Mine kwa hatua yake ya kuzalisha na kuchakata chumvi ghafi hadi kuwa bidhaa kamili sokoni, jambo ambalo linachangia kuongeza thamani ya rasilimali hiyo na kupunguza mzigo wa uagizaji kutoka nje ya nchi.
“Tasnia ya chumvi inaendelea kukua kwa kasi kila siku. Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hii, ili kuongeza tija na uzalishaji na kuondokana kabisa na uagizaji wa chumvi ghafi kutoka nje ya nchi kama malighafi ya viwanda,” ameongeza Waziri Mavunde.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Fred Milanzi, amesema kuwa uwepo wa Kampuni ya Nyanza Salt Mine wilayani humo umekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na mapato kwa Serikali pamoja na wananchi.
Ameeleza kuwa kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, jumla ya wananchi wapatao 1,000 wamepata ajira.
“Kupitia mradi huu, mapato ya Serikali yataongezeka kupitia kodi na malipo kwa wafanyakazi. Lakini pia, kwa kuwa tuna minada mingi ya mifugo wilayani hapa, uwekezaji huu wa chumvi lishe utasaidia sana mifugo, hasa ng’ombe, kupata madini ya chumvi muhimu kwa afya yao,” amesema Milanzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nyanza Salt Mine, Mukesh Mamlani, amesema kuwa uzalishaji wa bidhaa ya chumvi lishe itokanayo na madini ya chumvi ni mkombozi mkubwa kwa wafugaji wa Tanzania, na kwamba kampuni hiyo inalenga kuhakikisha inafikia malengo ya kuzalisha tani 120,000 za chumvi ifikapo mwaka 2027.

“Kwa kutekeleza malengo yetu, tayari tumeshafanya uwekezaji wa zaidi ya Sh20 bilioni.
“Hata hivyo, bado tunahitaji maeneo zaidi ya uwekezaji, hivyo tunaomba ushirikiano wa halmashauri katika kutupatia maeneo hayo ili kuongeza uzalishaji na kuchangia zaidi katika uchumi wa Taifa,” amesema Mukesh.