Rombo. Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza vyumba nane vya kulala wageni katika Hoteli ya Snow Cape, iliyopo eneo la Nalemuru katika Hifadhi ya Msitu North Kilimanjaro Rongai, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Hoteli hiyo ambayo ipo mpakani mwa Kenya na Tanzania imeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo, Agosti 25 na hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la moto na kusema chanzo chake hakijajulikana na uchunguzi unaendelea.
“Ni kweli Hoteli ya Snow Cape yenye vyumba nane vya kulala wageni iliyopo eneo la Nalemuru katika Hifadhi ya Msitu North Kilimanjaro iliyopo Rongai imeteketea kwa moto saa 10:00 usiku na hakuna binadamu aliyedhurika kwa moto huo,” amesema Kamanda Mkomagi.
Aidha, amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na kinachunguzwa na taarifa ya uchaguzi itatolewa hapo baadaye.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa ndugu wa mmiliki wa hoteli hiyo, Kenneth Salakana, amesema tukio hilo la moto limetokea wakati vyumba hivyo vikiwa havina wageni.
“Vyumba nane vyote vimeteketea kwa moto na bahati nzuri kulikuwa hakuna mtu ndani zaidi ni mali zimeteketea, bado hatujafahamu tatizo ni nini, wanachunguza,” amesema Salakana.