Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya Wilson Mbise (25), mkazi wa King’ori wilayani Arumeru na kujeruhi wengine sita.
Watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, wanadaiwa kutenda mauaji hayo Septemba 11, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Arusha, leo Ijumaa Agosti 15, 2025, ACP Salvas Makweli, amesema Wilson alifariki dunia katika msitu wa Mazingira uliopo Kijiji cha Muungano, kilichopo Kata ya King’ori.
Amesema pamoja na kutekeleza mauaji hayo pia waliwajeruhi watu wengine wanne sehemu mbalimbali za miili yao kwa tuhuma za wizi.
Kaimu amewataja waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Daud William (17), Kelvin Humphrey (22), Godbless Emmanuel (30) na Allen Nanyaro (21), wote wakiwa ni wakazi wa Kata ya King’ori.
“Aidha tunaendelea kukamilisha upelelezi wa tukio hilo,pindi utakapokamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha kwa uchunguzi wa daktari,” amesema.
“Jeshi la Polisi Arusha linawaonya baadhi ya watu wanaojichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha mila kuacha mara moja tabia hiyo, pindi wanapowakamata watuhumiwa watoe taarifa kwa vyombo husika ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa,” ameongeza.