Gharama ya uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo kushuka hadi Sh100,000

Dodoma. Serikali imetangaza kuwa kutokana na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya afya nchini, hasa kupitia Bohari ya Dawa (MSD), gharama za uchujaji damu (dialysis) kwa wagonjwa wa figo ziko mbioni kupunguzwa zaidi hadi kufikia Sh100,000 au chini yake kwa kila huduma moja.

Kwa sasa, gharama hiyo imefikia Sh200,000 kwa mara moja, ikilinganishwa na Sh360,000 zilizokuwa zikitozwa awali, kabla ya maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Agosti 15, 2025 akiwa kwenye ofisi za MSD, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hilo linawezekana kutokana na idadi ya mashine za kuchuja damu kuongezeka kwenye hospitali hapa nchini.

‎‎‎Msigwa amesema Serikali inatekeleza mpango maalumu wa huduma za uchujaji wa damu kwa mtu aliyepata athari za figo kiasi kwamba zinashindwa kuchuja damu.

‎‎”Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita hadi kufikia Agosti, 2025 idadi ya mashine  za kuchuja damu imeongezeka kutoka mashine 60 hadi 137 na hivyo kuongeza idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka MSD kutoka sita mwaka 2021 hadi kufikia hospitali 15 kwa mwaka 2025 uwekezaji huu umegharimu kiasi cha Sh7.7 bilioni,” amesema Msigwa

‎‎Amesema hospitali 11 ambazo zimepokea mashine hizo na zimeanza kutoa huduma ni pamoja na  hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es salaam ya Amana, Mwananyamala, Temeke, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure (Mwanza), na hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Chuo Kikuu Cha Dodoma (Udom) huku hospitali nne zikiwa kwenye hatua ya matengenezo.

‎‎”Na sasa hivi gharama tumezipunguza sana kwa sababu uchujaji wa mara moja kwa sasa hivi wastani ni kama Sh200,000, lakini ndugu zangu wote mtakumbuka miaka michache iliyopita ilikuwa Sh230,000.

‎”Lakini tulipotoka kama miaka mitano iliyopita ilikuwa ni zaidi ya Sh300,000 mimi nakumbuka tulikuwa na ndugu yangu ambaye tulipokea huduma hii kwa Sh360,000 kwa mchujo mmoja na wakati mwingine mgonjwa anaandikiwa mara tatu kwa wiki, kwa hiyo unachukua Sh360,000 unazidisha mara tatu kwa wiki huyu mgonjwa utamtibuje kwa hiyo ilikuwa ni gharama kubwa,” amesema.

‎‎Amesema mikakati ya Serikali kupitia MSD waendelee kushusha gharama hadi zifike Sh100,000 au chini ya hapo na kwamba inawezekana  kama MSD itaagiza mashine hizo na hivyo mahitaji ya uchujaji wa damu halitakuwa hitaji la kifo bali watu wengi wataweza kumudu.

‎‎Ametoa wito kwa sekta binafsi kujenga viwanda vya kuzalisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili waweze kuihudumia Serikali kwa kuwa mnunuzi mkubwa wa dawa nchini ni Serikali.

‎‎Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukay amesema bohari hiyo bado ipo kwenye mchakato wa kuweka mifumo sawa ya kuuza dawa kwenye nchi za SADC na za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

‎‎Amesema mpaka sasa mchakato huo unaenda vizuri na utakapo kamilika MSD itaanza kuuzia dawa nchi wanachama wa SADC na kwamba mpaka sasa kuna baadhi ya nchi zimeshaanza kupata dawa kutoka bohari hiyo pamoja na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

‎‎Amesema kucheleweshwa kwa mchakato kumetokana na nchi hizo kutokuwa na mfumo mmoja wa manunuzi, hivyo wanaweka sawa jambo hilo ili litakapoanza mfumo utakaotumika kwa nchi zote uwe mmoja tofauti na sasa ambapo kila nchi inatumia mfumo wake.

‎‎Kwa upande wake meneja wa MSD Kanda ya Kati, Mwanashekhe Juma amesema bohari hiyo inahudumia mikoa ya Dodoma na Singida  ambapo jumla ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za kati 760 zinahudumiwa na Kanda hiyo.