Kilio cha wananchi kutembea masafa marefu sasa basi, vikianzishwa vituo vipya vya daladala

Unguja. Baada ya wananchi kupaza sauti zao wakilalamikia masafa marefu wanayotembea kwa kukosa vituo vidogo vya daladala kufika katika ya mji, Serikali imeweka vituo vya muda vya kushusha na kupakia wakati ukisubiriwa mpango wa muda mrefu.

Katika utaratibu uliokuwapo awali, daladala zilizokuwa zikitoka nje ya mji zilitakiwa kuingia na kushusha kituo kikuu cha daladala Kikwajuni, kisha kwenda moja kwa moja hadi Hospitali ya Mnazimmoja.

Licha ya utaratibu huo, asilimia kubwa ya wananchi wanaotoka nje ya mji kuingia mjini, huwa wanakwenda Darajani ambapo ndio katikati ya mji wa Zanzibar na bidhaa zote muhimu hupatikana katika eneo hilo, lakini katika utaratibu huo kituo cha daladala Kisonge na Tobo la Pili, ambavyo vipo karibu na eneo hilo vilikuwa vimeondolewa hivyo kuibua usumbufu mkubwa kwao.

Hata hivyo, baada ya wananchi kulalamikia mazingira hayo, Serikali imeweka vituo vya muda ambavyo vitakuwa karibu na kuwarahisishia kufanya shughuli zao kwa wepesi.

Akitangaza vituo hivyo leo Agosti 15, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana amesema, Kijangwani kitabaki kuwa kituo kikuu lakini wameruhusu vituo vidogo vya Kisonge, Jamhuri Garden (Kisiwandui) na kituo cha Darajani Kisha Hospitali ya Mnazimmoja.

Abiria wakisubiria usafiri baada kuanzishwa na kuzinduliwa kituo kipya cha daladala Jamhuri Garden (Kisiwandui) Unguja, Zanzibar.

“Vituo hivi tulivyoweka daladala haitatakiwa kupiga debe, itashusha na kupakia na kuondoka kwa dakika tatu, ikizidi hapo hatua zingine zitachukuliwa,” amesema Kitwana.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka zote zinazohusika ikiwemo Manispaa na Jiji, kukubaliana namna bora ya kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kuingia na kutoka mjini.

Hata hivyo, utaratibu huo utatumika kwa muda wakati Serikali ikiendelea na mipango ya muda mrefu ya kuweka usafiri imara wa kutumia mabasi ya umeme katika mji huo.

“Lengo ni kuupangilia mji na kuondoa msongamano wa magari jambo linalokwamisha biashara zingine. Kwa hiyo Serikali imeliona hili na kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa,” amesema.

Nao baadhi ya wananchi wapengeza utaratibu huo wakisema walikuwa wanateseka kwani maeneo ya vituo vya daladala yalivyokuwa ilikuwa ni mateso.

Zuhra Khamis mkazi wa Kwarara amesema ilikuwa ni changamoto kubwa kwao mpaka ilikuwa inakatisha tamaa kufanya safari ya kwenda Mjini.

“Yaani Mjini ilikuwa inaonekana kama mateso, unajiuliza nafanyaje, kwani kutoka Kijangwani mpaka Darajani ni mbali sana wengine wanashindwa kutembea,” amesema.

Mwananchi mwingine aliyezungumzia jambo hilo ni Mohamed Ahmada mkazi wa Mwera ambaye amesema walikuwa wakiumia kwani ilikuwa wakitumia gharama kubwa kwa usafiri wa kuingia na kutoka mjini.

“Unalazimika kupanda bodaboda ama bajaji, kisa daladala hazifiki Mjini, lakini wengine hata hiyo fedha ya bodaboda hawana, kwahiyo unakuta inakuwa changamoto sana kwakweli,” amesema.

Mwingine Manono Ali Mohamed amesema; “Tunashukuru sana Mheshimiwa Rais amesikia kilio chetu sisi wanyonge maana yalikuwa ni mateso makubwa kukosa huduma hii muhimu.

“Unaweza kuona shida tuliyokuwa tunapata, mtu anashuka kwenye boti bandarini analazimika kutembea kwa miguu mpaka Kijwangani (takribani kilometa tatu) kwa ajili ya kupanda daladala aende anapokwenda, yalikuwa mateso makubwa.