Dodoma. Chama Cha NCCR-Mageuzi leo kimevunja rekodi kati ya vyama vilivyochukua fomu za kugombea kiti cha Rais kwa kuwa na idadi ndogo ya wasindikizaji.
Mgombea wa NCCR-Mageuzi Haji Ambar Khamis na mgombea mwenzake wake, Dk Evaline Munisi waliingia Ofisi za INEC wakiwa na wasindikizaji 11.
Miongoni mwa waliowasindikiza alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bara Joseph Selasini ambaye walimtangaza kuwa ndiye mgombea mwenza.
Wakati wanatoka ndani ya ukumbi, gari nyingine ndogo ilikuja na watu saba waliovalia mavazi ya sare za chama hicho na kuungana nao.
Akizungumza na wanahabari, mgombea huyo amesema ajenda yake kuu itakuwa ni maadili.
“Maadili yameporomoka sana,nchi imekosa maadili na kila mmoja anajiona kuwa na ndevu lazima tukakomeshe hilo,” amesema Khamis.
Mgombea huyo amewataja baadhi ya wasanii akisema wanatunga nyimbo za ajabu kwamba zinaharibu kizazi cha leo.
Kwa mujibu wa Khamis, NCCR-Mageuzi wakikabidhiwa nchi, ndani ya siku 100 watakamilisha mchakato wa Katiba Kwa haraka na kuanza kufanyia kazi.
Kuhusu kwa nini wamebadirisha mgombea mwenza, amesema ni utaratibu baada ya kuona wenzao CCM wamechukua Mwenyekiti na Katibu Mkuu kwa Jinsia.
“Kwanza tuliangalia Jinsia, lakini tunakwenda katika ushindani tukasema mbona CCM wamechukua viongozi wa juu, nasi tukafanya hivyo sasa tuko vizuri na mnamuona aliyekuwa mgombea mwenza (Joseph Selasini) yuko mstari wa mbele kwenye jambo hili,” amesema Khamis.
Katika hoja ya Afya ambayo imekuwa ikitajwa na wagombea wengi, ameeleza kwamba lazima wafanye maboresho na kuondoa alichokiita afya kugeuzwa chacho cha ukusanyaji mapato.