KIUNGO mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mganda Peter Lwasa anaingia Tanzania leo ili kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara , huku akiziingiza vitani Mtibwa Sugar na Pamba Jiji ambazo zimeonyesha nia ya kumtaka nyota huyo.
Hata hivyo, wakati Lwasa akiwaniwa na klabu hizo, taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kiungo huyo yupo katika mgogoro mzito na waajiri wake Kagera Sugar, kwa kile anachodai mwenyewe yupo huru na wala hana mkataba na kikosi hicho.
Kiungo huyo aliyejiunga na timu hiyo Agosti 15, 2024 akitokea KCCA ya Uganda, alisaini mkataba wa miaka miwili na kikosi hicho, ingawa amewataarifu viongozi mwaka mmoja uliobaki umevunjika kwa sababu ya Kagera Sugar kushuka daraja.
Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti, Kagera imefikia makubaliano na Mtibwa ya kumpata mchezaji huyo kwa msimu mzima kwa kile wanachodai bado pia ana mkataba, ingawa Lwasa amesimamia msimamo wake wa kudai ameshamalizana nao na yupo huru.
Mwanaspoti linatambua kwamba licha ya makubaliana hayo, lakini taarifa zinaeleza Pamba Jiji inamshawishi ajiunge nayo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha alichowekewa mezani ambacho ni tofauti na maslahi atayopewa Mtibwa Sugar msimu ujao.
“Mkataba wake na Kagera ni wa miaka miwili na amebakisha mmoja, yeye anasema baada ya timu kushuka ameshamalizana nao jambo ambalo sio kweli, tunatambua Pamba inamshawishi sana ila tutapambana ili kupata haki yetu,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lwasa alisema anatarajia kuwasili muda wowote kuanzia sasa hapa Tanzania ingawa suala zima la kubaki Kagera Sugar au kuondoka litategemea na makubaliano ya pande mbili watakayofikia, hivyo ni ngumu kuweka wazi.
Nyota huyo alifunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, akiichezea URA na KCCA zote za Uganda, Sofapaka, Kariobangi Sharks na Gor Mahia za Kenya, huku akiitumikia pia timu ya Lubumbashi Sports ya DR Congo.