ELIMU NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAWAFIKIA WANAWAKE MKOANI MBEYA KUPITIA KONGAMANO LA WANAWAKE NA FURSA ZA KIUCHUMI.

Mbeya.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetoa wito kwa wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia na kuchagua nishati safi kama njia ya kulinda afya, mazingira na kuimarisha uchumi wa kaya.

Akizungumza Agosti 15 katika kongamano la wanawake na wajasiriamali kuhusu fursa za kiuchumi lililofanyika mkoani Mbeya, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Deo Alex.

Amesema kuwa mwaka 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa maelekezo ya kuandaliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia,Kufuatia agizo hilo, Wizara ya Nishati iliandaa mkakati huo na kuuzindua rasmi mwaka 2024, na utekelezaji wake umeanza rasmi.

Kwa mujibu wa mkakati huo, matumizi ya nishati isiyo safi yameonekana kuwa chanzo kikuu cha athari mbalimbali, ikiwemo uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya kwa watumiaji, miongoni mwa athari za kiafya zilizobainishwa ni pamoja na saratani, homa za mapafu, mimba kuharibika, na kujifungua watoto kabla ya muda.

Ameeleza kuwa gharama za kumtibu mtu mwenye saratani ni kubwa sana ukilinganisha na gharama ya ununuzi wa nishati safi kama vile mtungi wa gesi, hivyo wananchi wanahimizwa kuwekeza katika matumizi ya nishati salama kwa ajili ya afya zao na mazingira, amebainisha kuwa mkakati huo umefungua fursa mbalimbali kwa wajasiriamali, ikiwa ni pamoja na kuwa mawakala wa gesi na nishati nyingine mbadala. 

Amezitaja aina za nishati safi zinazopendekezwa ni pamoja na umeme, gesi na mkaa mbadala n.k,  amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi yanapunguza gharama za matibabu na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jafari Haniu, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, amesema kuwa Mkoa wa Mbeya umejaliwa kuwa na fursa nyingi za kiuchumi kama kilimo, biashara, mifugo na uvuvi.

Amebainisha kuwa kupitia kongamano hilo, wanawake watapata nafasi ya kutambua fursa zilizopo katika mazingira yao, kuwafahamu wadau mbalimbali, pamoja na kupata uelewa kuhusu taratibu za ununuzi wa umma kupitia mfumo wa NEST, aidha amehimiza uundwaji wa vikundi kupitia halmashauri ili wanawake waweze kunufaika na fursa hizo.

Amesema hadi kufikia Juni 2025, Mkoa wa Mbeya umefanikiwa kuanzisha jumla ya majukwaa 544 ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika ngazi ya vijiji na mitaa, 149 katika kata, 5 katika wilaya na jukwaa 1 la ngazi ya mkoa, Vikundi 1,162 tayari vimejiunga na majukwaa hayo na baadhi yao wameweza kupata mikopo kupitia mifumo rasmi, ametoa rai kwa wanawake kuendelea kujiunga na vikundi ili kunufaika zaidi na fursa hizo ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye nishati safi ya kupikia.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Anastaz Mpanju, alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuwajengea uwezo wa kujipatia kipato, kuziwezesha familia zao na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, likiwa na kauli mbiu isemayo “Changamkia Fursa, Jenga Leo na Kesho Yako.”