CHAN 2024: Afrika Kusini yalia na VAR

TIMU ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ imebidi kusubiri mechi za mwisho za kundi C baada kutoka suluhu dhidi ya Niger huku ikilalamikia VAR mara mbili.

Huko Afrika Kusini kwa sasa mjadala ni namna ambavyo teknolojia hiyo ilivyowatibulia ushindi wa pili – matokeo ambayo yameifanya kuwa na pointi tano sawa wa Algeria inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Katika mechi dhidi ya Niger kwenye dakika ya 18, mwamuzi wa Morocco, Bouchra Kerboubi aliamuru penalti baada ya kumuona mchezaji wa Niger akishika mpira ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, baada ya kupitia kwenye VAR alibatilisha uamuzi wake. Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika lilitokea tukio lingine ambalo liliwafanya Afrika Kusini washinikize mwamuzi atazame VAR muda wa nyongeza. Tukio hilo pia haikuonekana kuwa ni penalti.

Licha ya kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, vijana wa kocha Murphy Ntseki walishindwa kuufungua ukuta wa Niger.

“Tulicheza vizuri, tulitawala mchezo, lakini hatukufanikiwa kutengeneza mabao muhimu,” alisema kocha Ntseki baada ya mechi akionyesha kutoridhika.