Maelfu waomba mikopo elimu ya juu kidijitali

Unguja. Miezi miwili baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuanza kutumia mfumo wa utambulisho wa barua za makazi kidijitali, tayari maombi 489,409 yameombwa kidijitali.

Bodi hiyo ilianza kutumia mfumo huo Juni 15, 2025 ambapo waombaji wanatakiwa kuwasilisha barua zao za makazi kwa njia ya kidijitali.

Haya yamebainishwa leo Agosti 16, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati wa utambulisho wa matumizi ya mfumo wa anwani za Makazi (NaP) kwa upande wa Zanzibar.

“Kuanzia Juni 15, 2025 mfumo umeanza kutumiwa na bodi waombaji wa mikopo kuwasilisha barua ya utambulisho kwa ukaazi kidijitali hadi sasa jumla ya maombi hayo yameombwa kidijitali,” amesema Slaa

Amesema mfumo huu unawaondolea wananchi usumbufu wa kutembelea ofisi za mitaa vijiji, “kwa hiyo ni matarajio yetu baada ya uzinduzi huu tunaongeza matumizi ya utambuzi kutumia dijitali.” 

Unapotekelezwa uchumi wa kidijitali, kwa mujibu wa Waziri Silaa, haliwezi kuachwa nyuma suala la anwani na makazi kwani mfumo huu unajenga misingi utakaowaleta pamoja wadau na kukuza uchumi wa Taifa.

“Kwa mantiki hiyo, hatuna budi kuwahusisha wadau mbalimbali ambao wanaweza kuwa mabalozi katika mfumo huu,”

Amesema wanatarajia kujenga uwezo wa watendaji wakiwemo masheha na kuwezesha upatikanaji wa vishikwambwi na kuhamasisha wadau kutumia mfumo katika shughuli za kila siku.

“Katika kufikia azma hiyo, wizara imeandaa mpango wa miaka miwili kuhakikisha waratibu na watendaji wote 21,487 wa mikoa na halmashauri zote Tanzania Bara na visiwani wanapatiwa vishikwambwi.

Kati ya hao waratibu 92 wa Mikoa, 390 wa halmashauri, watendaji  3656 wa kata 4,269 wa mitaa, 12,333 wa vijiji, 110 wa wadi na 388 wa shehia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema mfumo huo utachochea uchumi na kuimarisha ulinzi na usalama

Hemed amesema mfumo huo wa anwani za makazi sio tu utaonekana katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali, bali pia katika kuendeleza na kukuza sekta ya utalii na sekta nyingine.

“Wananchi na wadau wengine wana kila sababu ya kutumia mfumo huu ili kusaidia kupatikana kwa huduma mbalimbali ninawahamasisha wananchi kutumia programu hii kwa kuweka kwenye simu janja na maeneo mengine itasaidia katika ufanisi wa kutekeleza majukumu ya kila siku,” amesema Hemed

“Haya ni mageuzi makubwa katika kutoa huduma za kidijitali, jambo la muhimu kila mwananchi anapaswa kuwa amesajili katika mfumo huu ambao ni daftari la kidijitali.

Ameonywa wahalifu wanaong’oa nguzo na mabango ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kutambua maeneo huku akiagiza Ofisi ya Wizara Ujenzi na Tawala za Mikoa kuwajengea uwezo watendaji katika matumizi ya mfumo huo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kazi ya kuweka anwani ni endelevu ambapo kwa Zanzibar wameweka anwani 450,124 kwenye mitaa na viwanja.

Amesema ili mfumo huo uweze kufanya kazi vizuri zaidi, zipo kazi zinahitajika kufanyika kwa kushirikiana na wadu wote.

“Kwanza ni kuunganisha anwani hizo na mifumo ya kidijitali, pia kuziunganisha na mifumo ya utoaji wa huduma za posta za biashara na utoaji wa taarifa wakati wa dharura,” amesema

Amesema lazima waunganishe mifumo ya kifedha na usafiri na usafirishaji, kwakuwa miji inajengwa, barabara zinajengwa hivyo ipo haja ya kuhuisha taarifa hizo na mifumo ya uendeshaji na mifumo ya upigaji kura

Katibu Mkuu Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Habiba Hassan Omar amesema awali walianza na Shehia nne za majaribio, na tathmini imeonyesha kuna mafanikio makubwa.

Amesema watatoa vishikwambwi kwa masheha wote ambapo utavitumia katika kutoa barua za utambulisho kwa kidijitali.

“Wananchi wanapaswa kupata anwani za makazi kwa wale ambao hawajapata wajitahidi kwani ndio zitakazokuwa zinatumika katika utambulisho.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed amesema hatua hiyo italeta mageuzi makubwa ya utoaji huduma.

Katika kuliendea vyema jambo hilo, tayari serikali imeanza kujenga ofisi za masheha, kwa sasa zimeshajengwa ofisi 60 na zingine 147 zinaendelea kujengwa na malengo ni kufikia mwaka 2026 ziwe zimejengwa ofisi zote 388.

“Uwepo wa Ofisi hizi utasaidia utoaji wa huduma kwa wananchi hususani katika kipindi ambacho wanakwenda kutumia mfumo huo wa kidijitali, wananchi wajenge mazoea ya kuanza kujitambulisha kupitia anwani,” amesema Masoud.