Rais Mwinyi ataja mambo 4 akishawishi wananchi kuunga mkono uwekezaji

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kisiwani hapa kuunga mkono jitihada za uwekezaji wa utalii kwa kutaja sababu nne ikiwemo kukuza uchumi wa nchi, ajira, kupata soko kwa bidhaa za ndani na kodi kwa serikali.

Dk Mwinyi amesema uwepo wa miradi mikubwa ya hoteli nchini inasaidia kuongeza idadi ya watalii ambao wanasaidia kuongeza uchumi kwa wananchi. Ameyasema hayo leo Jumamosi Agosti 16, 2025 katika ufunguzi wa hoteli ya Zan Breeze Beach Resort iliyopo Kikungwi, Mkoa wa Kusini Unguja. 

“Natoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada za uwekezaji wa utalii kwa sababu tunapataka kukuza uchumi wa nchi, ajira, kupata soko kwa bidhaa za ndani na kodi kwa serikali,” amesema Dk Mwinyi 

Dk Mwinyi, amesema kwa sasa hadhi na taswira ya utalii imebadilika kwa kasi,  kutokana na hali hiyo imesababisha kuchipuka kwa miradi mingi ya ukodishaji nyumba kupitia mitando na watoa huduma.

Amesema, Serikali imeweza kuvutia uwekezaji katika sekta ya hoteli ambapo jumla ya miradi 202 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni mbili imesajiliwa na mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar,  Shariff Ali Shariff(kushoto) akimuonesha kitu Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati akikagua hotel ya Zan Breeze Beach Resort.

Amefafanua, miradi hiyo imechangia ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka watalii 260,644 mwaka 2020 hadi watalii 736,755 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 64.6.

“Kati ya miradi 202 iliyosajiliwa miradi 105 ipo katika Mkoa wa Kusini Unguja, hii ni ishara kuwa Mkoa huu umefunguka kiutalii,” amesema 

Sambamba na hilo, Dk Mwinyi amesema Serikali imeweza kutunga sheria mpya ya Uwekezaji ya Zanzibar mwaka 2023 ambayo imefanikiwa kuwalinda wawekezaji wazalendo kwa kuwawekea viwango vidogo vya mtaji ili  kuwekeza katika sekta ya utalii.

Ameseme, Sheria hiyo inawatambua wote ambao uwekezaji wao unafikia thamani ya dola laki moja kuwa wawekezaji wazalendo tofauti na awali ambapo mwekezaji mzalendo alitakiwa awe na mtaji usiopungua dola laki tano katika sekta ya utalii na dola laki tatu katika sekta nyengine za kiuchumi. 

Amefahamisha kuwa, hali hiyo imefungua milango kwa wazawa wengi kuweza kushiriki kikamilifu katika biashara ya utalii na hatimaye kuchangia kwa utekelezaji wa sera nchini.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka  Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema mradi huo umegharimu Sh10bilioni, vila sita zenye vyumba 33, migahawa miwili yenye uwezo wa kuhudumia wageni 70, bwawa kubwa la kuogelea, eneo la mazoezi na ukumbi wa mikutano.

Amesema, mradi huo ni  kati ya miradi 512 iliyosajiliwa kipindi cha miaka mitano na ambapo mradi huo una hadhi ya nyota tatu yenye gharama ya dola za kimarekani bilioni sita, miradi yote hiyo inategemea kuzalisha ajira 26,000 kwa wananchi.

Mwekezaji wa mradi huo, Prite  Ashok amesema hoteli hiyo imekuja kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya eneo hilo kwani ina lengo kuongeza thamani ya uchumi wa nchi.

Amesema, mradi huo umeanza kwa kuwajali wanakijiji cha Kikungwi kwa kuwasogezea huduma za kijamii ikiwemo miundombinu ya barabara na kuboresha shule inayotumiwa wakazi hao.

“Huu ni ukurasa mpya kwa wakazi wa eneo hili kwa sababu tunawajali na tutahakikisha tunatatua changamoto zao kwa kushirikiana pamoja hivyo mradi hii upo kuongeza thamani ya uchumi kwa wananchi hao,” amesema Ashok.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema mradi huo umeleta sura mpya kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuboresha mandhari ya eneo hilo kuwa katika taswira nzuri.