NSSF YATOA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KATIKA KONGAMANO LA WANAWAKE KUHUSU FURSA ZA KIUCHUMI MKOANI MBEYA

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeshiriki na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa washiriki wa kongamano la Wanawake kuhusu fursa za kiuchumi mkoani Mbeya ambalo limeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ikiwa na kauli mbiu isemayo “Changamkia Fursa, Jenga Leo na Kesho Yako”

Akifungua kongamano hilo la wanawake na wafanyabiashara wadogo wa mkoa huo, lililokuwa na lengo la kutoa elimu ya kutambua na kuchangamkia fursa za kiuchumi; Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema, zaidi ya vikundi 3,000 vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vimesajiliwa na serikali mkoani Mbeya ndani ya mwaka mmoja, huku vikundi 736 vikinufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri mkoani humo.

Haniu amesema vikundi hivyo vilisajiliwa ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025 na baadhi ya vikundi vimejiunga kwenye majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayopatikana kwenye ngazi mbalimbali.

Akizungumza katika kongamano hilo Rehema Chuma, Meneja wa wanachama waliojiajiri wenyewe alikuwa miongoni mwa waliotoa mada katika kongamano hilo, amesema kuwa NSSF inaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na wananchi waliojiajiri wenyewe ambapo sekta hiyo inajumuisha makundi mbalimbali kama vile wanawake wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wavuvi, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine wote ili waweze kujiunga na kuchangia katika Mfuko kwa maisha yao ya sasa na baadaye.

Sambamba na hilo, NSSF imeshiriki kongamano hilo kwa lengo la kuendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla ikiwemo elimu kuhusu mafao, jinsi ya kujisajili kwa wanachama wapya kutoka sekta binafsi na wananchi waliojiajiri wenyewe pia elimu ya jinsi wanavyoweza kujichangia kupitia simu ya mkononi popote walipo na elimu kuhusu huduma za kidijiti (NSSF Portal).