Geita. Wazazi wametakiwa kuacha tabia ya ‘kufuga’ watoto kwa kuwapa chakula na mavazi pekee badala ya ‘kulea’ kwa kuwajengea maadili na kuwasaidia watu bora wenye uwezo wa kujisimamia na kuwa na maisha mazuri ya baadaye.
Akizungumza wakati wa mahafali ya nne ya Shule ya Msingi Ave Marie iliyopo Mjini Geita, Padri wa Kanisa Katoliki Geita, Alphonce Twimanyekwenye amesema malezi ya mtoto ni sawa na kuendesha gari ambapo mzazi analazimika kutumia “gia zote” ikiwemo upole, ukali, kuonya, kusamehe na kuadhibu pale inapobidi.
“Mtoto si mali ya mzazi bali ni mali ya Mungu, kila mzazi ataulizwa amemlea vipi mtoto, kwa sasa wazazi wengi hamlei ila mnafuga na ndio maana watoto wa sasa hivi kila mzazi analalamika lakini mnasahahu aliyekosea kwenye malezi ni mzazi mwenyewe,” amesema.

Padri Twimanyekwenye pia amewashauri wazazi kuacha kuwatukana watoto kwa kuwaita majina ya wanyama kwani inaharibu roho zao na kutahadharisha wazazi kutowatuma watoto pombe au sigara, kwa kuwa ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili.
“Maneno yana nguvu uwe mwangalifu unapoyatumia acheni kuwapa watoto kila wanachoomba hata kama unacho mfundishe kuwa kuna kupata na kukosa acheni kuwarahisishia dunia maana dunia sio rahisi akikuwa anashindwa kukubaliana na maisha ya kujitegemea,” amesema Padri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Andrew Mathias amesema taasisi hiyo ambayo pia inafundisha lugha za Kifaransa na Kichina imelenga kuwaandaa wanafunzi na changamoto za ajira na utandawazi.

Naye mkuu wa shule hiyo, Bilishi Luzalia amesema changamoto kubwa inayowakabili ni pamoja na wazazi kutofuatilia maendeleo ya watoto na kushindwa kuhudhuria vikao vya shule, hali inayochelewesha jitihada za walimu kuinua kiwango cha taaluma.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Lucy Beda amewataka wahitimu hao kuendelea kuwa wasikivu na wenye nidhamu hata wanapoendelea na masomo ya sekondari.
“Nidhamu na heshima mliyokuwa nayo shuleni iendelee nyumbani. Wasikilizeni wazazi kama mnavyowasikiliza walimu ili muwe watoto wenye tabia njema. Pia epukeni kujiunga na makundi mabaya yatakayowaharibia maisha,” amesema Beda.
Aidha, amewataka wazazi kufundisha watoto kazi za nyumbani kipindi hiki cha likizo ndefu,sanjari na kushirikiana na walimu kupiga vita utoro kwa wao kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kufanikisha ndoto za kielimu.