Ujenzi SGR Uvinza – Musongati waiva

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshiriki uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza hadi Musongati, akiwahakikishia Watanzania na Warundi kwamba, ujenzi huo utaanza katika muda uliopangwa.

Majaliwa ameshiriki hafla hiyo iliyofanyika eneo la Musongati, nchini Burundi leo Agosti 16, 2025 akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema reli hiyo yenye urefu wa kilomita 240 ikikamilika itakuwa ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Majaliwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi.

“Reli ikikamilika itafungua fursa kwa wananchi ambao wataweza kutoka hapa hadi Dar es Salaam ndani ya siku moja. Hata kwenye usafirishaji wa mizigo, hivi sasa lori linatumia saa 96 kutoka Dar hadi Bujumbura lakini baada ya kukamilisha ujenzi, usafirishaji wa mizigo kwa kutumia treni utatumia saa 20 tu,” amesema Majaliwa kama alivyonukuliwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Mradi wa reli ya kisasa siyo tu kwamba utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, bali pia utafungua milango ya fursa mpya za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Burundi,” amesema.

Amesema ujenzi wa reli hiyo utagharimu Dola bilioni 2.154 za Marekani na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano. Mwaka mmoja baada ya ujenzi ameeleza utakuwa wa matazamio.

Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimiye amesema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli.

“Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza,” amesema.

Amesema Burundi imebarikiwa kuwa madini mengi na kuna wakati aliitisha kikao cha wawekezaji kutoka nchi kadhaa, wengi wakavutiwa na wakataka kuwekeza mara moja, lakini wakamuuliza wakianza kuchimba madini ya nikeli watayasafirishaje.

“Hiyo changamoto ilitufanya tubungue bongo zetu na kutafuta suluhisho.  Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuungana nasi ili tuanze mradi huu muhimu. Tukitoka hapa, tunataka reli iunganishe hadi Kindu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na baada ya hapo, tunataka reli yetu ifike Afrika Magharibi kwenye ufukwe wa bahari ya Atlantiki kwani tunaamini njia hiyo itaharakisha kuleta maendeleo,” amesema.

Amempongeza Rais Samia kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo akisema:

“Nimekaa Tanzania kwa muda mrefu lakini kwa sasa nikija naweza kupotea. Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti napajua, Mwenge napajua na Kinondoni nilishakaa; lakini kwa sababu ya maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake imara.”

Kauli hiyo aliizungumza kwa Kiswahili na kuamsha shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.

Awali, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alieleza utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na Ajenda 63 ya Umoja wa Afrika ambayo inataka Bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa reli ya kisasa.

Amesema mbali na kuziunganisha nchi hizo mbili, kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutarahisisha kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo.

“Hivi sasa, kontena moja la futi 20 linasafirishwa kwa gharama ya Dola 3,800 lakini reli ikikamilika, gharama itashuka hadi Dola 2,000,” amesema.

Amesema faida nyingine itakayopatikana baada ya mradi huo kukamilika ni kuwezesha kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja. “Hivi sasa, mzigo unaosafirishwa kwa lori moja ni tani 30, lakini reli ikianza kazi, tutaweza kusafirisha tani 3,000 kwa wakati mmoja,” amesema.