Mbeya. Katika kuhakikisha huduma bora za uangalizi wa watoto walizaliwa kabla ya muda, Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya imenufaika na vifaa tiba vya kisasa (Monitor) 15 kutoka kwa Wadau wa Maendeleo Tanzania.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo Jumamosi Agosti 16, 2025 na Meneja wa Kampuni ya Goal 3 Tanzania, Mwamvua Mika kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Mbeya,Dk Myriam Msalale.
Amesema vifaa tiba hivyo tayari vimefungwa na kuanza kutoa huduma lengo ni kuhakikisha watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wanapata huduma bora kama sehemu ya kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita katika kugusa sekta ya afya.
“Tumefunga vifaa tiba vya kisasa kwenye kitengo cha Niku ili kuboresha huduma kwa watoto wachanga ,lakini pia tushukuru uongozi wa Hosptali kwa ushirikiano mzuri wa hatua kwa hatua hadi kufanikisha kufunga monitor 15 ambazo kimsingi zitaleta chachu kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma bora, “amesema.
Awali, akizungumza baada ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Myriam Msalale amewashukuru wadau kwa kuguswa kuchagia vifaa tiba vya kisasa ambavyo vitahochea uboreshwaji wa huduma kwa watoto wachanga walio kwenye uangalizi .
Amesema kimsingi vimekuja wakati mzuri na kwamba vitaleta tija katika kuboresha huduma kwa watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda, lakini pia nisisitize vitumike kwa uangalizi mkubwa.
“Nitake tu vitaatiba hivyo kwa kisasa ambavyo leo tumekabidhiwa na wadau wa maendeleo visimamiwe vyema ili viweze kudumu kwa muda mrefu katika kuboresha huduma ya watoto wanao zaliwa kabla ya muda na kufikishwa kwenye kitengo hicho,”amesema.
Daktari Bingwa mbobezi wa watoto wachanga, Dk Rehema Marando amesema vifaa tiba hivyo vitaleta tija kubwa ya kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma za matibabu na uangalizi kwa watoto.
“Kimsingi sasa huduma zitaboreshwa zaidi lakini tunashukuru wadau wa maendeleo kwa hatua hiyo nzuri ya kugusa na kuongeza ufanisi wa vifaa tiba kwa ajili ya watoto wachanga kikubwa tunashukuru, “amesema.
Mkazi wa Soko la Matola jijini hapa, Rehema Mwanjonde amesema hatua ya wadau kugusa huduma za afya kwa watoto wachanga ni ishara kubwa ya ushirikiano na serikali iliyopo madarakani na kuomba wengine kuguswa kuchangia ili kunusuru vifo visivyo vya lazima.