Mfaransa atoa ‘code’ ya kiungo Yanga

MFARANSA Julien Chevalier amempa maujanja kocha wa Yanga Romain Folz, jinsi ya kumtumia Celestin Ecua, huku akiwatobolea Simba siri ya Djessan Privat.

Julien alikuwa kocha wa Ecua katika timu ya Asec Mimosas akimfundisha kwa kipindi cha nusu msimu – akimpokea kutoka Zoman ya hukohuko Ivory Coast.

Ecua ambaye ametua Yanga akijiandaa kukichezea kikosi hicho msimu ujao amesaini mkataba wa miaka mitatu.

Akizungumza na Mwanaspoti kocha Julien alisema mashabiki wengi wanaposikia Ecua ni mshambuliaji, basi wanadhani anacheza namba tisa, jambo ambalo sio sahihi.

“Kwanza Ecua sio namba tisa labda achezeshwe kama namba kumi au atokee pembeni huko ndio atakuwa hatari, japokuwa nafasi zote anazicheza kwa ubora,” alisema Julien.

“Namuelewa sana Ecua kwa kipindi nilichomfundisha na nafasi inayomfanya awe huru zaidi ni pale anapocheza akitokea pembeni kuliko kumbana kama namba tisa kamili.”

Ikumbukwe kuwa, miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuhitajiwa na Simba ni Djessan ambaye anaichezea Zoman FC katika nafasi ya ushambuliaji.

Inadaiwa kwamba anasikilizia dili Msimbazi iwapo straika Leonel Ateba ataondoka katika kikosi hicho, ambapo kwa sasa inaelezwa mpango huo uko mbioni.

Akimzungumzia Djessan kocha Julien alisema anamfahamu vizuri kutokana na ligi wanayocheza kuwa ni moja ndio maana akaujua ubora wake.

“Simba kama itampata Djessan basi watakuwa nao wamepata mtu bora wa kucheza kama Ecua kwani naye ni hatari zaidi  na anajua kufunga.

“Djessan ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo mshambuliaji, akijulikana kwa nguvu, kasi, na maamuzi sahihi akiwa na mpira.

“Ana uwezo mzuri wa kupenya kati ya mabeki na mara nyingi hutengeneza nafasi za mabao kwa pasi za mwisho zenye ubunifu na ana nguvu za kutosha kushindana, pamoja na uwezo wa kufunga,” alisema kocha Julien.

Ecua na Djessan ni mastaa ambao wamewahi kucheza timu moja msimu uliomalizika (Zoman), lakini baada ya dirisha dogo mmoja alitimkia Asec Mimosas.

Wote walimaliza na idadi ya mabao sita kila mmoja, huku Ecua akiachana na Zoman akiwa ameifungia mabao saba ndani ya nusu msimu kabla ya kwenda Asec Mimosas.