Vita ya namba 10 Simba, Ateba akiaga

KWENYE kikosi cha Simba imezuka vita mpya hata kabla ya kiungo mshambuliaji Neo Maema hajatua kambini na mabosi wa timu hiyo sasa wanakuna kichwa.

Maema juzi alikamilisha dili lake la kujiunga na Simba akitokea Mamelodi Sundowns ukiwa ni usajili wa pili Simba wanaufanya kutoka kwenye kikosi hicho ambacho msimu uliopita kilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni sahihi kusema kuwa huyu ndiye mchezaji mwenye wasifu mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Simba kwa sasa na mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kuona makali yake.

Hata hivyo, ujio wake kwenye kikosi hicho ambacho kina ukame wa mafanikio umeanzisha vita mpya na kiungo Jean Charles Ahoua ambaye alionyesha makali msimu uliopita na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kutupia mabao 16.

Vita yao siyo ya namba uwanjani, bali ni namba ya jezi, kwani kwa sasa Ahoua anavaa namba 10 ambapo inaelezwa kuwa Maema naye ameshaueleza uongozi wa timu hiyo kuwa ndiyo namba yake kipenzi na angependa kuitumia msimu ujao.

Chanzo cha uhakika kutoka kwenye kikosi cha Simba nchini Misri kimesema uongozi wa timu hiyo kwa sasa unakuna kichwa kuhakikisha kuwa unawaweka wachezaji hao chini ili kupata suluhu ya jambo hilo, mara tu baada ya nahodha huyo wa Afrika Kusini kwenye kikosi kinachoshiriki Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), atakapotua kambini.

“Kazi iliyopo sasa ni kuwaweka chini na kumuomba Ahoua jezi namba 10 ili tumpatie Maema ambaye ameiomba kuivaa akitua kikosini mara baada ya kumaliza michuano ya CHAN 2024 inayoendelea Tanzania, Kenya na Uganda,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Ni kazi ngumu kwa kuwa huyu mchezaji msimu uliopita alifanya kazi nzuri na ni chaguo la kocha, siyo kila mchezaji huwa anakubali kuachia jezi yake. Sijafahamu itakavyokuwa endapo akigoma, lakini naona kuwa kuna kazi kubwa haswa hapa.

“Ukiondoa ombi hilo nyota huyo kwenye mkataba wake kuna kipengele cha kupewa bonasi na Sh30 milioni endapo atahusika kwenye mabao 15, haya ninaelezwa ni makubaliano yao na uongozi.”

Maema aliagwa na wababe hao wa Sauzi baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio katika kipindi cha miaka minne.

Mchezaji huyo ndani ya Sundowns ameshinda mataji saba yakiwemo manne ya Ligi Kuu Afrika Kusini, moja Kombe la Nedbank na jingine la MTN8 mbali na ubingwa wa African Football League (AFL).  Katika miaka minne kiungo huyo akiwa Mamelodi amecheza mechi 120 akifunga mabao 13 na kutoa asisti 14.

Kiungo huyo atajiunga na Simba mara baada ya kumalizika kwa fainali za CHAN akiwa tayari ameshafunga bao moja katika kikosi cha Afrika Kusini..

Wakati Maema anaingia kwenye kikosi hicho, taarifa inasema kuwa mshambuliaji Leonel Ateba juzi aliondoka kambini kumpisha staa huyo ambaye anaweza kucheza kiungo wa kati, kulia na kushoto. Simba ipo jijini Cairo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya 2025/26 wa Ligi Kuu Bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Sina hakika ni timu gani amemalizana nayo ila ninachoweza kusema ameaga na ameondolewa kwenye mfumo kupisha usajili wa Maema, lakini kuna timu anajiunga nayo kwa kuwa mazungumzo yalikuwa yakiendelea,” kilisema chanzo.