LEO Agosti 17 kuna mtanange wa kukata na shoka kwenye Uwnaja wa Nyayo jijini Nairobi kati ya timu ya taifa ya Morocco na DRC Congo kwenye Kundi A ambazo zinatafuta nafasi ya kufuzu robo fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kwenye kundi hilo Kenya inaongoza ikiwa na pointi saba na tayari imeshafuzu kwa hatua ya robo fainali. Morocco iko nafasi ya pili na pointi sita sawa na DRC Congo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mshindi kati ya Morocco na DRC Congo ataungana na Kenya ambao wanahitaji alama moja tu kujiweka salama kileleni mwa Kundi A, na ushindi utawapeleka robo fainali kama vinara bila kutegemea matokeo mengine.
Ni mechi inayozikutanisha timu zilizofanya vizuri mechi iliyopita; Morocco ambao baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Zambia wamejirudia kwenye ubora wao kimbinu, na DR Congo ambao mechi iliyopita walishinda mabao 2-0 dhidi ya Angola huku ulinzi wao ukiwa imara ukiruhusu bao moja kwenye mechi tatu.
Hivyo, ushindi kwa timu yoyote unamaanisha kufuzu moja kwa moja, lakini timu hizo zikitoka sare kutategemea na matokeo ya Kenya vs Zambia. Ikiwa Kenya itashinda, sare itawapa Morocco nafasi kwa tofauti ya mabao.
Mshambuliaji wa Morocco, Youssef Mehri alisema: “Tuko tayari kwa mchezo unaofuata dhidi ya DR Congo, kwa lengo la kufuzu hatua ya kwanza, ambalo kwa sasa ndilo lengo letu kuu. Lengo la kufuzu hatua ya robo fainali linabaki kuwa shabaha yetu kuu kwa sasa,” alisema na kuongeza:
“Hatukuanza vizuri michuano hii na tumeona makosa tuliyoyafanya mechi zilizopita na sasa hatutaki kurudia tena, hivyo tutapambana kuvuka hatua hii na tunajua ugumu wa mchezo huo.”
Kocha wa DR Congo, Otis N’Goma alisema: “Tunahitaji ushindi kwenye mechi hiyo ili kufuzu na tunafahamu ugumu ukikutana na timu kama Morocco. Ushindi wa mechi mbili mfululizo umeongeza morali na tunaamini tutapata pointi tatu.”
Timu zote mbili zimeangusha pointi tatu mbele ya mwenyeji Kenya zikichapwa bao 1-0, kisha Morocco ikashinda 2-0 dhidi ya Angola na 3-1 dhidi ya Zambia, huku DRC baada ya kichapo na Harambee Stars ikishinda 2-0 dhidi ya Zambia na Angola.