Morocco: Yeyote aje tu robo fainali

KOCHA wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amejivunia ubora wa kikosi huku akisema vijana wake wana uwezo wa kushindana na timu yoyote katika hatua ya robo fainali ya michuano CHAN.

Stars ilitinga robo fainali ya michuano hiyo ikiwa na mechi moja mkononi iliyokamilishwa jana Jumamosi usiku dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kudumisha rekodi nzuri katika msimamo wa kundi B baada ya kuzifunga Burkina Faso (2-0), Mauritania (1-0) na Madagascar (2-1).

“Tumepata nafasi ya kufuatilia kwa ukaribu mechi za wapinzani wetu kwenye kundi A ikiwemo Kenya, DR Congo na Morocco maana bado hatujajua moja kwa moja tutacheza na nani,” alisema Morocco.

“Naamini kabisa kwa ubora wa vijana wangu na motisha wanayoionyesha tuna uwezo wa kushindana na yeyote atakayekuja mbele yetu. Robo fainali ni hatua ngumu pengine kuliko makundi, haijalishi unakutana na mpinzani wa aina gani tutafanya maandalizi kwa ukubwa ili kuwapa raha Watanzania.”

Bado haijafahamika Stars itakabiliana na timu ipi kutokana na kupishana kidogo kwa pointi kulikopo kati ya kinara – Kenya mwenye alama saba, Morocco sita sawa na DR Congo.

Mechi za mwisho kwa kundi A leo Jumapili ndizo zitaamua nani atakabiliana na Stars – mechi ambazo zitapigwa ni Kenya dhidi ya Zambia ambayo itakuwa ikikamilisha ratiba huku DR Congo ikicheza na Morocco zote kiisaka robo fainali.

Kama Kenya itashinda mechi ya mwisho, Stars itakabiliana na mashindi kati ya DR Congo au Morocco na kama itapoteza basi itakutana na Stars huku mshindi wa mechi kati ya DR Congo au Morocco ataongoza kundi hilo. Ikiwa mechi zote zitaisha kwa sare, Stars itakutana na Morocco kwenye hatua hiyo Agosti 22 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.