BAADA ya aliyekuwa beki wa kati wa Tabora United, Mkongomani Andy Bikoko Lobuka kumaliza mkataba na kikosi hicho, mabosi wa Dodoma Jiji wamefungua mazungumzo na nyota huyo ili kuitumikia msimu ujao.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Tabora United msimu wa 2023-2024 akitokea SM Sanga Balende ya kwao DR Congo amemaliza mkataba wa miaka miwili na kikosi cha ‘Nyuki wa Tabora’ na sasa mabosi wa Dodoma Jiji wanaiwinda saini yake.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza Bikoko amewekewa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho, ingawa suala la maslahi binafsi kati ya pande zote mbili ndilo limekuwa changamoto ya kufikia muafaka.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema usajili unaofanyika kwa sasa wameliachia benchi jipya la ufundi, hivyo watazingatia ripoti iliyofikishwa mezani kwa kuifanyia kazi haraka zaidi.
Hata hivyo, licha ya Dodoma kumuwekea mkataba mezani nyota huyo, mabosi wa Tabora United walikuwa wanapambana ili kubaki naye msimu ujao, japokuwa changamoto imekuwa suala la kuboreshewa maslahi tofauti na aliyokuwa anapewa.
Bikoko licha ya kucheza beki wa kati, pia ana uwezo mzuri wa kufunga ambapo msimu wake wa kwanza (2023-2024) akiwa na Tabora United aliifungia mabao matatu, huku ule wa 2024-2025 alimaliza na mabao mawili.