Idadi ya watalii wa matibabu wanaokuja nchini imeongezeka mara mbili kati ya mwaka 2021 hadi 2025, hatua iliyochangia kuingiza Shilingi bilioni 116.5 katika pato la taifa, kutokana na ongezeko la asilimia 19 katika sekta ya utalii tiba.
Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Diplomasia kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi John Ulanga, wakati wa mdahalo wa wazi wa kitaaluma kuhusu utalii tiba ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Balozi Ulanga alisema idadi ya wagonjwa waliokuja kutibiwa nchini imeongezeka kutoka 5,700 mwaka 2021 hadi kufikia 12,180 mwaka 2025. Wagonjwa hao wanatoka katika nchi 16 za Afrika, huku Comoro ikiongoza kwa kutoa wagonjwa 2,770, Burundi ikiwakilisha asilimia 46 ya idadi hiyo, Zambia asilimia 8, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) asilimia 10, na Kenya asilimia 4.
“Kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, tumeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa nje wanaokuja kutibiwa hapa nchini kupitia taasisi kama JKCI, MOI, Muhimbili, Benjamini Mkapa na Ocean Road. Awali lengo lilikuwa kupunguza rufaa za nje kwa Watanzania, lakini sasa tumeweza kuvutia wagonjwa kutoka nje,” alisema Balozi Ulanga.
Aidha, alibainisha matarajio ya kuwa na wagonjwa 30,000 wanaokuja kutibiwa nchini ifikapo mwaka 2030, idadi hiyo ikitarajiwa kufikia 68,000 mwaka 2040 na wagonjwa 120,000 mwaka 2050.
Kuhusu mchango wa sekta hiyo kiuchumi, alisema mapato ya sasa kwa mwaka 2025 yanakadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 65, ambapo ifikapo mwaka 2030 mapato hayo yanatarajiwa kuwa Dola milioni 200, mwaka 2040 kufikia Dola milioni 420 na hatimaye Dola milioni 850 mwaka 2050.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mdahalo huo, alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa na mipango madhubuti ya serikali katika sekta ya afya.
“Tunataka Tanzania iwe kitovu cha huduma za matibabu barani Afrika. Tayari tumeandaa muongozo wa utalii tiba na kupitia Samia Scholarship tunaendelea kufadhili wataalamu wa kada mbalimbali ili kuboresha huduma zaidi,” alisema Dk. Shekalaghe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema kwa sasa asilimia 99 ya wagonjwa wa moyo nchini wanatibiwa ndani, hali iliyosaidia kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 95 ambazo zingetumika kuwasafirisha nje ya nchi.
“Tumefikia mikoa 23 kupitia mpango wa Samia Suluhu Hassan Outreach, tumezindua vituo vya huduma Kawe, Mikocheni na Arusha, na tumeingia ubia na Hospitali ya Seliani kwa ajili ya huduma za moyo. Hivi sasa tunapanua huduma hadi Chato,” alisema Dk. Kisenge.
Aliongeza kuwa tayari wamewafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa 14,000, upasuaji mkubwa na mdogo kwa wagonjwa 6,000 na kutoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa wa nje 900,000.
Katika hatua nyingine, alisema taasisi hiyo inatarajia kuanzisha hospitali ya moyo visiwani Comoro pamoja na kujenga hospitali maalum ya moyo kwa watoto katika eneo la Mloganzila.
“Katika wiki mbili zijazo tunaanza programu mpya ya matibabu kwa wagonjwa wa shinikizo la damu sugu. Huduma zitaendelea kupanuka ili kuimarisha nafasi ya Tanzania kwenye sekta ya utalii tiba,” alibainisha Dk. Kisenge.
Mwisho.