Shujaa wa Tabora Anayeandika, Kupika na Kufua kwa Miguu – Video – Global Publishers

Wakazi wa Tabora wanaomfahamu Bahati Iddi Nzimano (45) humuelezea kama mfano wa uvumilivu na uthubutu wa kuishi maisha kwa masharti yake mwenyewe.
Bahati, mkazi wa nyumba namba 14 Barabara ya Lumumba, eneo la Gongoni karibu na Chuo Kikuu cha SAUT, anaishi na mama yake mwenye umri wa miaka 75 anayehitaji uangalizi wa karibu kutokana na uzee.

Tofauti na wengi, Bahati alizaliwa bila mikono na hutumia miguu yake kufanya shughuli zote za kila siku.

KAZI ZA MIGUU
Kwa ustadi wa hali ya juu, Bahati humimina chai, kuandika, kupika na kufanya usafi kwa kutumia vidole vya miguu. Anasema hajawahi kuiacha hali yake iwe kikwazo cha kuendelea kuishi maisha ya kawaida.

Wapo watu hupoteza hata kidole kimoja tu na kukata tamaa, lakini Bahati amekabiliana na dunia si kwa mikono, bali kwa miguu yenye ustadi na dhamira ya chuma. Kila jambo ambalo wengi hulifanya kwa kikono, kama vile— Kupika, kumimina chai, kuandika, kufua nguo, kufanya usafi — yeye hufanya kwa kutumia vidole vya miguu yake, vikiongozwa na nia isiyokubali kushindwa.

UMAARUFU
Umaarufu wake ulianza mwaka 1995 alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mihayo. Wakati huo, marehemu Jonas Marios, mpiga picha wa Daily News, alimwona akiandika daftari kwa kutumia mguu na kupiga picha iliyopamba ukurasa wa mbele wa gazeti hilo.

Unaweza kumsaidia kutimiza ndoto yake kupitia namba-:
+255 788 955 266