KATIKA kuhakikisha inafanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mabosi wa Mlandege wamemuongeza kocha Abdallah Mohamed ‘Baresi’ katika benchi la ufundi la timu hiyo.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Zanzibar imekata tiketi ya michuano tangu 2021 ikipangwa kukutana na Ethiopia Insurance ya Ethiopia kati ya Septemba 19 wataanzia ugenini.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Mlandege, Hassan Ramadhan Hamis, amesema wamemuongeza Baresi huyo kutokana na leseni aliyokuwa nayo ambayo itatusaidia kwenye michuano ya kimataifa.
“Ni kweli Baresi ni kocha aliyeungana nasi ndio maana umemuona uwanja wa mazoezi amekuja kuongeza nguvu ana Leseni A ambayo inamfanya akae benchi michuano ya kimataifa mimi nina B,” amesema Hamis na kuongeza;
“Ujio wake naamini utaongeza nguvu kikosini lakini, hata benchi langu la ufundi natambua ubora wake naamini atakuwa chachu ya sisi kufanya vizuri na kuondoa dhana ya kuondoka hatua za awali katika michuano ya kimataifa.”
Akizungumzia maandalizi kwa ujumla amesema wanaendelea vizuri na wamefanya usajili mzuri ambao wanaamini utaweza kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri ndani na kimataifa.
“Ni kweli tumepoteza nyota zaidi ya wanne baada ya kuisaidia timu kutwaa taji lakini hilo haliondoi kufanya vizuri timu ina vipaji vingi lakini pia tumesajili nyota wengi ambao tunaamini wataipambania nembo ya timu.”