Bwana Yesu asifiwe naitwa Mwalimu George Mbwambo kutoka Dar es salaam Karibu kwenye mahubiri ya siku ya Leo yenye kichwa kinachosema ‘Namna amani ya Kristo inavyofanya kazi kwenye maisha ya mtu”
Kila mwanadamu hutamani kuishi maisha ya utulivu, usalama na furaha ya kweli. Lakini mara nyingi dunia hii hujaa misukosuko, hofu na mashaka. Watu wengi hutafuta amani kupitia mali, heshima, madaraka au hata burudani, lakini yote haya huwa ni ya muda mfupi.
Biblia inatufundisha kwamba amani ya kweli hupatikana kwa Kristo pekee. Yesu alisema: “Amani nawapa, amani yangu nawapa; si kama vile ulimwengu utoavyo, mimi nawapa ninyi” (Yohana 14:27). Hii ndiyo amani ya Kristo amani isiyofifia kwa sababu ya hali, bali inayotokana na uwepo wa Mungu ndani ya moyo wa mtu.
Wafilipi 4:7* “Na amani ya Mungu ipitayo akili zote italinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Amani ya Kristo inapotawala maisha yako mambo yafuatayo yanatokea ndani yako:-
Inaondoa hofu na wasiwasi kwenye maisha yako
Katika hali ya magumu, amani ya Kristo hutuliza moyo. Yesu alisema: “Msifadhaike mioyo yenu…” (Yohana 14:27). Hutoa utulivu hata bila majibu ya haraka.
Inakuongoza kufanya maamuzi sahihi
Wakolosai 3:15: “Amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu…”. Amani huwa kama hakikisho au onyo la rohoni. Ukikosa amani, subiri au omba zaidi.
Amani huleta umoja katika mahusiano
Kristo ni “Amani yetu”. Waefeso 2:14.Katika familia, ndoa au kanisa, amani huponya migogoro.
Amani hujenga imani ya ndani
Inapokuwa na amani, moyo huamini zaidi hakuna mashaka wala haraka zisizo za kiroho. Mfano: Yesu alipokuwa kwenye mashua wakati wa dhoruba alikuwa na amani, usingizi wake ulionyesha uaminifu wake kwa Mungu (Marko 4:37–39).
Amani hufungua mazingira ya kusikia mungu
Mungu hunena kwa sauti ya utulivu (1 Wafalme 19:12). Mahali pa amani pana wepesi wa kupokea ufunuo na uongozi wa Roho Mtakatifu. Nninachokuombea Kwa Mungu amani yake ndani yako.
Hata hivyo wewe unayesoma ujumbe huu wa neno la Mungu, unapaswa kufahamu kwamba amani ya Kristo ni matokeo ya msamaha wa dhambi.
Kabla ya mtu kumpokea Yesu, moyo wake huwa mzito kwa sababu ya dhambi na hatia. Dhambi hutenganisha mwanadamu na Mungu na kusababisha hofu ya hukumu. Lakini Yesu Kristo alikufa msalabani ili kuondoa ile enzi ya uadui kati ya Mungu na wanadamu. Warumi 5:1 inasema: “Basi tukiisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.”
Hivyo basi, amani ya Kristo huanza kwa kukiri dhambi na kumpokea Yesu kama Mwokozi. Hapo mtu hupata uhuru wa dhamira, na hofu ya hukumu hubadilishwa kuwa furaha ya wokovu.
Amani ya Kristo huleta utulivu wa ndani
Dunia ikikumbwa na machafuko, mtu mwenye Kristo ndani ya moyo wake hubaki mtulivu. Paulo aliandika: “Na amani ya Mungu ipitayo akili zote na iwe mlinzi wa mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:7). Amani hii si matokeo ya kutoona matatizo, bali ni uwezo wa Mungu kumpa mtu nguvu ya kustahimili changamoto bila kuvunjika moyo.
Mfano ni Paulo na Sila walipokuwa gerezani, waliimba nyimbo za kumsifu Mungu badala ya kulia kwa mateso yao (Matendo 16:25). Hii ni nguvu ya amani ya Kristo ikifanya kazi.
Amani ya Kristo hubadili mahusiano ya mtu na wengine
Mtu anayebeba amani ya Kristo hubadilika pia katika jinsi anavyoshirikiana na jirani. Efe 2:14 inasema: “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tulio wawili kuwa mmoja…” Kristo hufuta chuki, kinyongo na visasi kati ya watu.
Mtu mwenye amani ya Kristo hujifunza kusamehe, kupenda na kuvumilia wengine. Ndiyo maana Yesu alisema “Heri wapatanishi; kwa maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9). Kupitia amani ya Kristo, familia huwekwa mbali na ugomvi, makanisa hujengwa katika upendo, na jamii hubadilishwa kwa mshikamano.
Amani ya Kristo hutoa ujasiri na matumaini
Amani ya Kristo si tu kwa maisha haya, bali pia kwa maisha yajayo. Yohana 16:33 Yesu alisema: “Katika ulimwengu mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Hivyo, mtu anayemwamini Kristo hukabiliana na hofu za kesho kwa imani.
Hata kifo hakimpi hofu, maana amani ya Kristo humhakikishia uzima wa milele. Stephano shahidi wa kwanza, alikufa akiwa na uso ulioangaza kama wa malaika kwa sababu moyo wake ulijawa na amani ya Kristo (Matendo 7:54-60).
Amani ya Kristo ni zawadi ya kipekee ambayo dunia haiwezi kutoa. Kila mmoja wetu anaweza kuipokea leo kwa kumwamini Yesu Kristo na kuruhusu Roho Mtakatifu kutawala ndani ya mioyo yetu.
Yesu ndiye chanzo cha amani ya kweli, na anayempokea kamwe hataishi tena katika hofu, bali katika utulivu, furaha na matumaini tele.