LILE straika la Azam FC, Japhet Kitambala limeendelea kutuma salamu kwa mbali likiwa kule Kenya, huku kocha Mkongomani akitoa tahadhari kwa timu za Ligi Kuu Bara kuwa zijipange kwelikweli kukabiliana na mshambuliaji huyo.
Kitambala amesajiliwa na Azam dirisha hili la usajili akitokea Union Maniema ambayo awali ilimchukua akitokea TP Mazembe ambapo mara baada ya kumalizika kwa fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ataungana na kambi ya timu yake hiyo mpya.
Katika mechi tatu ambazo Kitambala amecheza CHAN ametengeneza bao na kufunga moja, DR Congo ikiwa kundi A lililopo Kenya.
Lakini, Kocha Mkongomani Raul Shungu ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kwamba Azam imepata mshambuliaji mzuri anayekwenda kuungana na kocha anayemjua vizuri – Florent Ibenge.
Shungu alisema hana shida na Kitambala kwenda Azam kwa kuwa mshambuliaji huyo ana msingi mzuri wa kumudu ligi ya Tanzania kutokana na kuwa na nguvu ya kupambana na beki yeyote.
“Nimeona Kitambala amesajiliwa na Azam. Naona anakwenda kuungana na baba yake – Ibenge. Unajua wachezaji wengi hapa Congo wana heshima kubwa na Ibenge. (Kitambala) ni mshambuliaji mzuri Azam wamepata.
“Kitambala atafanya vizuri. Unajua hapo Tanzania ili mchezaji aweze kucheza sawasawa anatakiwa aweze kutumia sana nguvu na akili, hivyo vitu Kitambala anavyo. Huyu ni mchezaji anayeweza kuweka kichwa pale ambapo beki ameweka mguu. Anajituma sana uwanjani. Anaweza asifunge, lakini akatengeneza nafasi mwingine akafunga,” alisema Shungu.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga alisema mshambuliaji huyo sasa anatakiwa kuhakikisha anajiimarisha anaongeza kasi ya kutumia nafasi kwa kuwa anahamia timu ambayo inataka matokeo.
“Azam naona wanajenga timu imara, wamepata kocha mkubwa na sasa wanataka wachezaji wakubwa, anachotakiwa (Kitambala) ni kuongeza juhudi kwenye kufunga kwa kuwa mabeki hawatamsumbua kwa nguvu atawaweza,” alisema Shungu.
Azam FC iko katika maandalizi ya msimu ujao, huku ikijipanga kuondoka Karatu kwenda Rwanda ambako itakaa wiki mbili, huku ikiwakosa baadhi ya mastaa ambao wako kwenye majukumu ya timu ya Taifa.