Mohamed Rashid atajwa Fountain Gate

UONGOZI wa Fountain Gate (FG) uko katika mazungumzo kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mohamed Rashid ‘Mo Rashid’ baada ya kukubaliana maslahi binafsi na kilichobaki kwa sasa ni kusaini kandarasi.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zimelidokeza Mwanaspoti kwamba Mo Rashid amekubaliana maslahi binafsi na tayari amepewa mkataba wa miaka miwili wa kukitumikia kikosi hicho kuanzia msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema msimu ujao wanataka kufanya mambo makubwa zaidi tofauti na uliopita, hivyo hadi sasa kuna majina ya nyota wapya ambao wanaendelea na mazungumzo nao na watawaweka wazi.

“Msimu uliopita hatukufanya vizuri na presha ya kushuka daraja unaona jinsi ilivyokuwa kubwa. Sasa hatuhitaji tena kuona linatokea. Tunaendelea na vikao vyetu vya bodi ya wakurugenzi na tukikamilisha tutaweka wazi hilo,” alisema Wendo.

Aliongeza kuwa msimu uliopita ulikuwa kipimo sahihi kwao kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza, hivyo presha waliyopitia ya kuinusuru timu hiyo hawataki ijirudie ndio maana wanataka kukisuka tena upya kikosi hicho.

Mo Rashid ni miongoni mwa washambuliaji wazoefu ambao wanakumbukwa zaidi msimu wa 2017-2018 alipofunga mabao 10 ya Ligi Kuu Bara na kushika nafasi ya tano akiwa na Tanzania Prisons huku akiwahi pia kuichezea JKT Tanzania.