Kocha Mlandege afichua dili ya usajili wa Yakoub Msimbazi

WAKATI ikitajwa kuwa kipa namba moja wa JKT Tanzania na timu ya taifa,  Taifa Stars,  Yacoub Suleiman kuwa kamalizana na Simba kocha aliyemuibua nyota huyo, Hassan Ramadhan Hamis amekiri kuwepo kwa mazungumzo ya dili hilo.

Hata hivyo, amesema kuwepo bado hajui kinachoendelea, ila kipa huyo amehakikishiwa nafasi na Fadlu Davids endapo mambo yataenda vizuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hamis amesema ni kweli Simba wameonyesha nia ya kumnasa kipa huyo na kumpa mkataba kwa ajili ya kusaini, lakini kuna mambo hayajakaa sawa dili hilo kufikia mwisho.

“Nikiwa JKU ambayo ndio ilimuuza Yacoub mpango wetu ulikuwa ni kumsajili kaka yake lakini baada ya kwenda kufanya mazungumzo na wazazi wake mama yake ndio alituambia kaka mtu ni mgonjwa hivyo akatupa mdogo wake ambaye ndio huyo anafanya vizuri sasa,” alisema kocha Hamis na kuongeza;

“Ni kipa mzuri, nakiri kuwa familia yao kuwa na makipa wazuri kwa sababu kaka yake alikuwa na kipaji kikubwa ndio maana tulishawishika kumfuata baada ya kubaini ana shida ndio sababu ya kuibuka kwa Yakoub ambaye ni kipa mzuri.”

Amesema kipa huyo ni bora kutokana na kuwa mwanafunzi siku zote akiweka wazi, amekuwa mtu wa kijifunza kila siku na anamuona akiwa Tanzania One miaka ijayo kwenye nafasi anayocheza.

“Nafurahi amekuwa akiaminiwa na shida ambayo inamfanya awe na wakati mgumu kutua Simba ni kuhofia kupoteza namba kikosi cha Taifa Stars, lakini kocha wa Simba, Fadlu Davids kamhakikishia nafasi ya kucheza.”