Chipukizi yafyeka 10 Ligi Kuu Zanzibar 

KIKOSI cha Chipukizi United kinachoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, kimefyeka wachezaji 10, huku ikiendelea kujisuka upya kwa kunasa saini za nyota watano na kutupia jicho michuano ya CHAN ili kujenga kikosi hatari kwa lengo la kupambania kutwaa mataji yote ya ndani.

Chipukizi iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita ikimaliza nafasi ya tisa kati ya timu 16 zinazoshiriki ZPL, imesema imefyeka nyota hao ili kuongeza nyota wengine ambao wataiweka timu hiyo katika ushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Chipukizi, Kheri Kidema alisema wamenipanga vizuri kwa msimu ujao, licha ya kuachana na baadhi ya wachezaji 10, lakini  mipango yao ni kusajili nyota wengine kumi.

“Tayari tumesajili watano, ambayo tayari wameshaungana na timu kujiandaa na msimu mpya bado tunafanya jitihada ya kuangalia nyota wengine kupitia michuano ya CHAN 2024 inayoendelea lengo ni kujenga kikosi bora cha ushindani,” amesema Ofisa Habari huyo na kuongeza;

“Tumejipanga vizuri baada ya kushindwa kufikia malengo msimu uliopita, tukishindwa kutetea taji la FA baada ya kucheza fainali huku katika ligi tukiponea chupuchupu kushuka daraja.”

Amesema wanafahamu haitakuwa rahisi kwao kufikia malengo hayo bila ya mipango, lakini wanaamini usajili waliofanya utakuwa chachu ya ushindani ligi ya ndani.

Nyota walioachwa na Chipukizi yenye maskani visiwani Pemba ni;  Abbas Ali Abbas, Izhaka Yakub Wazir, Peny Sabastian
Vuai, Makame Jecha Ibrahim, Mohammed Salum Mganga, Abubakar Muhsin Joka,
Frank Bossa (under 20), Haruna Thomas Soko, Baraka Elias Baraka na 
Yussuf Makame Chande.