Mkazi wa jijini Mwanza, Pendo Zephania anasema miongoni mwa vitu anavyopenda kufanya kwa mwenza wake, ni kumlalia ubavuni karibu na eneo la kwapa, huku akisema anavutiwa na harufu ya eneo hilo anayodai inampa utulivu, amani na kumrahisishia kupata usingizi.
“Napenda harufu ya mwenza wangu…nahisi amani na utulivu hali ambayo husababisha nipitiwe na usingizi kirahisi,”anasimulia.
Anachosema Pendo kinaweza kutofautiana na watu wengi wanaoamini kuwa mvuto kati ya wapenzi hutegemea maneno matamu, mguso wa kimahaba au hata mwonekano wa nje.
Hata hivyo, wasichojua watu hawa na hata kukifikiria ni kama jasho la mwenza wako linaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuondoa msongo wa mawazo, kukuza mapenzi, na hata kuimarisha kinga ya mwili wako.
Hii si dhana isiyo na mashiko, ni ukweli unaotiwa nguvu na kazi za utafiti wa kisayansi. Ni kazi zinazofichua maajabu na siri iliyojificha kwenye harufu ya miili yetu.
Mwaka 2018, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha British Columbia (UBC) nchini Canada, walifanya utafiti wa kuvutia ulioongozwa na Profesa Frances Chen.
Katika utafiti huo, wanawake walitakiwa kunusa fulana zilizovaliwa na wenza wao au watu wasiowajua. Matokeo yalionyesha kuwa wanawake waliovuta harufu ya jasho la wapenzi wao walipata upungufu mkubwa wa homoni ya msongo wa mawazo iitwayo cortisol.
Hii ilidokeza kuwa harufu ya mwenza inaweza kuleta hisia za utulivu na usalama, hata ikiwa hayupo karibu kimwili.
Katika utafiti mwingine uliochapishwa kwenye jarida la Scientific American mwaka 2007, wanasayansi katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, walichunguza athari za kemikali ya androstadienone (sehemu ya harufu inayopatikana kwenye jasho la wanaume) na kubaini kuwa harufu hiyo iliweza kuongeza kiwango cha homoni ya cortisol kwa wanawake na kuongeza hisia za furaha na msisimko.
Kemikali hiyo pia ilihusishwa na kuimarika kwa mhemko wa wanawake waliokuwa wakinusa majasho ya wenza wao.
Kwa upande wa mvuto wa kimapenzi, kazi za kitafuti zilizofanywa na Claus Wedekind, mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Bern, Uswisi, mwaka 1995 zilionyesha kuwa wanawake huvutiwa zaidi na harufu ya wanaume wenye tofauti kubwa ya vinasaba vinavyohusiana na kinga ya mwili.
Daktari katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Dk Joseph Chacha anasema japo suala hilo si la kitabibu, mtu kupenda harufu ya mwingine si jambo geni na hutokea mara nyingi kwa watu walio kwenye uhusiano.
“Suala la harufu lina depend (inategemeana) kama wewe umemzoea mpenzi wako na unampenda hata akiwa na harufu mbaya huwezi kuona kama kuna shida, na ukiisikia ile harufu pengine kwa sababu unampenda unaweza kujikuta inakuondolea stress (msongo),’’ anaeleza.
Jasho na hisia za furaha, woga
Zaidi ya hayo, wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Utrecht nchini Uholanzi, waligundua kuwa hisia kama furaha au woga zinaweza kuambukizwa kwa njia ya harufu ya jasho.
Katika utafiti wao wa mwaka 2015, waligundua kuwa wanawake waliweza kutambua kama jasho la mtu lilitokana na hali ya furaha au woga, na hata kuathiriwa kihisia kulingana na hali hiyo. Hii inaonesha kuwa jasho si tu kiashiria cha mvuto wa kimapenzi, bali pia njia ya mawasiliano ya kihisia.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2023 na watafiti wa taasisi ya Karolinska nchini Uswisi, ulionyesha kuwa kunusa harufu za jasho la mtu mwingine kunaweza kusaidia kupunguza wasiwasi wa kijamii.
Katika utafiti huo, sampuli za jasho kutoka kwa watu waliotazamwa wakihisi hisia tofauti zilitumika kutibu wanawake 48 waliokuwa na hofu ya kijamii, huku baadhi yao wakipokea tiba ya utulivu wa akili (mindfulness therapy).
Matokeo yalionyesha kuwa wanawake waliopokea tiba ya utulivu pamoja na harufu ya jasho walipunguza kiwango cha wasiwasi kwa asilimia 39, ikilinganishwa na asilimia 17 tu kwa wale waliopokea tiba bila harufu.
Hii ilionyesha kuwa harufu ya jasho inaweza kuongeza ufanisi wa matibabu ya wasiwasi wa kijamii, bila kujali aina ya hisia (furaha au hofu) wakati wa kutoa jasho.
Mtafiti mkuu, Elisa Vigna, alifafanua kuwa harufu ya jasho inaweza kuwa njia ya mawasiliano ya kihisia isiyo ya maneno inayosaidia kuleta hisia za utulivu na usalama kwa mgonjwa.
Sio wote wanavutiwa na harufu
Faida hizo za jasho zinategemea na jinsi unavyompenda na kumzoea mwenza wako. Nje ya hilo, harufu yake inaweza kuwa kinyume yaani ikachukiza badala ya kutuliza.
Dk Chacha anasema kwa wasio na uhusiano wa kimapenzi, hawawezi kufurahia harufu ya mtu mwingine, kwa kuwa hawana sababu ya kuifurahia bali huwa kero kwao.
“Yaani mtu ambaye tunategemea anaweza kupenda harufu bila sababu ni mama mjamzito tu kwa sababu yeye anaweza tu kuipenda hata bila sababu yoyote, lakini wewe mtu mzima tu upo vizuri hauna shida yoyote mimi nanuka makwapa unawezaje kunipenda?,” anahoji.
Jabir Kulwa anasimulia katika safari zake za uhusiano alishawahi kukutana na binti ambaye hawakudumu muda mrefu kwenye uhusiano huo kutokana na kushindwa kuvumilia harufu yake ya jasho.
“Pengine sikumpenda vya kutosha, lakini ukweli ni kwamba harufu ya jasho lake ilikuwa inaninyima raha. Wakati mwingine hata nikimkumbatia nilijikuta sipo huru, kumbatio lake nililiona kama kero,” anasema na kuongeza:
“Sasa nina mtu mwingine maishani mwangu. Yeye ana kajasho fulani hivi lakini ni laini, siyo kali. Nikimkumbatia, badala ya kero, napata hisia safi na za upendo.”
Ni muhimu kukumbuka kuwa kunusa jasho siyo hatari moja kwa moja kwa afya, lakini kugusana na jasho lenye bakteria au fangasi kunaweza kuwa hatari katika mazingira fulani.
Hivyo ni vizuri kwa wenza kuhimizana usafi wa mwili mara kwa mara.
Mwenza ana jasho kali linalokupa shida?
Kumwambia mpenzi wako kuhusu harufu ya jasho au usafi kunahitaji hekima, heshima, na upole, ili asiwe na maumivu ya kihisia au kuona kama unamkosoa vibaya. Jaribu kutumia njia hizi:
Anza kwa sifa au maneno ya upendo:
Usianze moja kwa moja na tatizo. Anza kwa kumpa uhakika wa mapenzi yako kwake.
“Napenda sana kuwa karibu na wewe, unaniweka huru na najisikia salama ukiwa karibu…”
Tumia lugha ya pamoja (“sisi” badala ya “wewe”): Hii husaidia kumfanya ajisikie kuwa unamshambulia, bali mnashirikiana.
“Najua wakati mwingine mwili wetu hutoa harufu hasa tukichoka au kuwa sehemu za joto. Nimekuwa nikihisi kuna wakati tungetumia manukato au kuoga kabla ya kuwa karibu zaidi ili tujisikie freshi kabisa…”
Toa suluhisho au pendekezo kwa upole: Badala ya kusema “una harufu mbaya”, unaweza kutoa wazo la kuboresha hali hiyo.
“Tunaweza tukajaribu kutumia sabuni au manukato fulani pamoja, au tuoge kabla ya kukutana kimapenzi. Nafikiri hiyo itafanya kila kitu kizidi kuwa kizuri zaidi.”
Mletee zawadi: Wakati mwingine unaweza hata kumletea zawadi kama manukato ya kupulizia,
sabuni ya harufu nzuri au mafuta yenye manukato.
Jasho ni maji yanayotolewa na tezi za ngozi ya binadamu ili kusaidia mwili kupooza na kudhibiti joto.
Husaidia kupooza mwili kwa asili pale inapohitajika mathalani wakati wa kufanya mazoezi au kukaa kwenye jua kali ili kumwepusha mtu kupata joto kupita kiasi.
Mchakato wa jasho husaidia mwili kudumisha joto linalofaa, si la juu sana wala la chini mno ambalo kwa kawaida ni takriban nyuzi joto 37.
Zaidi ya kupooza, jasho pia ina kazi nyingine muhimu kama vile kusaidia kuimarisha unyevu wa ngozi na kuizuia kukauka.
Pia, jasho lina viambata vinavyopambana na vijidudu (antimicrobial peptides) ambavyo ni kemikali asilia zinazosaidia mfumo wa kinga wa mwili kuzuia maambukizi ya bakteria na fangasi yanayoweza kuingia kwenye ngozi.
Jasho lenyewe halina harufu, lakini linapokaa muda mrefu au kuchanganyika na bakteria walioko kwenye ngozi, ndipo linatoa harufu mbaya.
Mambo yanayosababisha mtu kutokwa jasho ni pamoja na joto la mazingira, mazoezi au kazi nzito, hofu, hasira, au msongo wa mawazo. Pia magonjwa fulani kama hyperthyroidism,kisukari na homa.