Mke wa mpenzi wangu ananitishia maisha

Nipo kwenye uhusiano na mume wa mtu kwa miaka mitano sasa. Katika huo uhusiano nimemsaidia sana mpenzi wangu kiakili na hata mipango,hadi amejenga nyumba anayoishi na familia yake na kusomesha watoto katika shule nzuri.

Nimemwingiza kwenye biashara na kumkutanisha na wafanyabiashara wakubwa kwa sababu mimi tangu kitambo ninafanya biashara ya mazao.

Kwa kweli nimemsaidia sana kubadili maisha yake na familia yake pia. Tulipokutana alianza kunilalamikia kuhusu mkewe kutokuwa mshauri mzuri hata akimpa pesa afanye biashara anazitumia vibaya, hapo ndipo tulipoanzia hadi kuwa wapenzi.

Kwa bahati mbaya mkewe amejua uhusiano wetu na ananitisha maisha na kunitambia akisema nimefuata pesa za mume wake mpaka nakosa raha, ilihali mimi ndiyo ninajua mafanikio ya familia yake yamepatikana vipi.

Sasa ninawaza nimtoe mumewe kwenye mrija wa pesa ili arudi alikotokea na mkewe atie akili kuwa wanawake wa nje siyo wote wachumia tumbo kuna wenye akili.

Ila kabla sijafikia huko naomba ushauri maana anaitishia sana maisha kwa kunitumia ujumbe, kutuma watu kiasi nahisi nipo hatarini.

Hapana hupaswi kupambana na mwenye mali, kwanza hukuwa sawa hata kidogo kuwekeza mapenzi, akili na kumpa moyo wako mume wa mtu. Hata kama umemsaidia kwa kiasi gani huyo anabaki kuwa mali ya mtu mwingine kihalali kabisa.

Kama huyo mwanaume angekuwa hampendi mkewe kutokana na sababu alizokupa mwanzoni angekuwa ameshamuacha, kama umeishi naye miaka mitano na bado yupo na mkewe inamaanisha yupo na wewe kwa muda tu utafikia wakati mtatengana.

Lakini kumbuka kuwa na uhusiano na mume wa mtu si jambo linalokupa heshima mbele ya jamii. Ni kama kukaa kwenye kiti cha basi cha mtu mwingine ukijua mwenye kiti yupo njiani akija utampisha na lawama juu. Atakufanyia visa vya kila aina huyo mwanamke na lawama zitakuja kwako kwa sababu ataonekana anadai haki yake inayopokwa na wewe.

Hatua yoyote ya kumchafua mumewe kwa sasa haitakufanya mshindi; badala yake inaweza kukugeukia kisheria na kijamii.

Pili, siri unazozijua ni zao la uhusiano uliojengwa gizani. Ukizitoa, unaivua heshima yako mwenyewe kwanza kabla ya yeye kuharibikiwa. Utakapotumia siri kama silaha, jamii haitakuona bingwa bali kama mchochezi. Na kumbuka, kuchafua wengine hakufanyi chuki zao kukoma; mara nyingi huchochea vita vipya visivyoisha.

Tatu, kujilinganisha na mke halali ni kujipoteza. Yeye yupo pale kwa mkataba wa ndoa, wewe upo kwa mkataba wa hisia unaoweza kuvunjika wakati wowote. Kumdharau kutakupeleka kwenye mashindano yasiyo na faida, kwani hata ushindi wake ni wa muda na una gharama kubwa kwa nafsi yako, usisahau huyu mke wa ndoa ana ulinzi kuanza kwenye familia yake, ya mumewe, viongozi wa Serikali na wa dini kushindana naye ni kujiumiza bure.

Kama unataka kumkomesha kweli na aache kabisa kukufuatafuata jitoe kwenye uhusiano huo na kujilinda kisheria dhidi ya vitisho vyake. Najua mazoea yana taabu, kuachana ghafla kutakuumiza na pengine utakuwa unakwenda mbele, unarudi nyuma lakini ukiwa na dhamira ya kweli utashinda. Ukiendelea kuushikilia uhusiano huu na vita hii, utabaki na vidonda visivyotibika.

Nakushauri jiondoe ukiwa mzima kuliko kubaki ukipigana vita vya mtu mwingine hadi uharibike. Kuna maisha nje ya kivuli cha ndoa ya mtu.