KOCHA wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema mechi ya jana usiku dhidi ya Afrika ya Kati ilikuwa ni kama darasa kwa wachezaji wa kikosi hicho, akibainisha wamepata somo ambalo anaamini litawasaidia katika maandalizi ya mechi ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024.
Taifa Stars ilimaliza mechi za makundi kwa suluhu dhidi ya Afrika ya Kati na kufikisha pointi 10 ikiongoza kundi ikifuatiwa na Madagascar iliyomaliza na alama saba kama Mauritania iliyotolewa.
“Ninachoshukuru ni kwamba tuliingia kwenye mechi ya mwisho ukiwa tayari tumefuzu robo fainali, ilikuwa ni jambo zuri sana kwetu, hivyo mechi dhidi ya Afrika ya Kati ilikuwa darasa, pamoja na kwamba wenzetu walioteza mechi zilizopita wanakikosi kizuri,” alisema Morocco.
Kocha huyo alisema ingawa walikosa ushindi wa nne mfululizo, wachezaji wake walionyesha kiwango kizuri huku wakitengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo walishindwa kuzitumia.
“Nilisema awali kuwa tutakutana na timu yenye nguvu na haingekuwa rahisi kushinda. Wachezaji wangu walifanya vizuri na niliwapongeza baada ya jitihada zao,” aliongeza.
Kuhusu safu yake ya ushambuliaji kushindwa kutumia vizuri nafasi, Morocco alisema; “Tunapaswa kuangalia upya mkakati wetu ili kufunga mabao katika mechi ya robo fainali.”
Kwa upande wa CAR, kocha Sébastien Ngato alieleza; “Nawapongeza wachezaji wangu kwa kulinda heshima yetu na kupata pointi. Tulicheza dhidi ya timu iliyo nyumbani na mbele ya mashabiki wake.”
Ngato aliongeza kwa kusema; “Ninafurahi kushiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza tangu uhuru wa nchi yetu.”
Kocha huyo alibainisha kuwa kikosi chake ni kichanga na bado kipo katika hatua ya kujifunza hivyo anaamini wakati mwingine watakuwa bora zaidi katika mashindano hayo.