Mastaa waliovuja jasho zaidi Taifa Stars

KATIKA mechi nne za hatua ya makundi ya mashindano ya CHAN 2024 ambayo yanaendelea ukanda wa Afrika Mashariki, ni wachezaji wanne tu wa Taifa Stars ambao wamevuja jasho zaidi kwa kucheza kila dakika ya mechi hizo.

Wachezaji hao ambao ni kipa, Yakoub Suleiman, mabeki wa kati, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wamecheza kwa zaidi ya dakika 360  katika mechi dhidi ya Burkina Faso, Mauritania, Madagascar na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Yakoub ambaye ni mchezaji wa JKT Tanzania amekuwa na mchango mkubwa kwa timu, akiruhusu bao moja tu kwenye mechi ya Madagascar na kuondoka na ‘Clean Sheet’ kwenye mechi tatu.

Hizi ni mechi za ushindi wa 1-0 dhidi ya Mauritania, 2-0 dhidi ya Burkina Faso, na suluhu dhidi ya CAR.

Kwa upande wa Job na Bacca, mabeki wa kati wa Yanga SC, wameendelea kuonyesha kiwango cha juu, wamekuwa wakiongoza safu ya ulinzi kwa nidhamu, wakifanya Taifa Stars kuwa miongoni mwa timu zilizoruhusu mabao machache zaidi kwenye hatua ya makundi.

Mbali na wachezaji hao, Fei Toto’ amekuwa kama uti wa mgongo wa Taifa Stars kwenye eneo la kiungo, amekuwa akifanya vizuri katika kuzuia na kuchezesha timu jambo ambalo limemfanya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara mbili.

Ameibuka mchezaji bora wa mechi dhidi ya Burkina Faso na CAR.