BAADA ya kuisaidia timu yake kutinga hatua ya robo fainali Michuano ya CHAN na akiibuka mchezaji bora, kipa wa Madagascar, Michel Ramandimbozwa ametaja siri ya timu yake kutinga hatua hiyo ni kumsoma mpinzani na kujiandaa vyema.
Madagascar imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 2-1, huku Ramandimbozwa akiitwaa tuzo ya pili ya nyota wa mchezo baada ya kufanya hivyo pia kwenye mchezo dhidi ya Maurtania mchezo ulimalizika kwa suluhu.
Akizungumza mara baada ya mchezo kumalizika alisema ilikuwa ni mipango yao kutinga hatua hiyo licha ya kuanza vibaya huku akifichua siri ya ushindi kuwa mbali na maandalizi mazuri waliyoyafanya walijipa muda kumsoma mpinzani wao.
“Burkina Faso sio timu mbaya una wachezaji wengi bora na ni timu ambayo inacheza kwa kasi na nguvu hilo tulilifahamu tunalifanyia kazi kabla ya kukutana nao mpango wetu ulifanikiwa kwa asilimia zote ndio maana tumepata matokeo,” alisema Ramandimbozwa na kuongeza;
“Benchi la ufundi limefanya kazi kubwa na sisi kama wachezaji tulikuwa na malengo sawa ndiyo maana tumefikia hapa, nawapongeza Burkina Faso walitupa mchezo mzuri na wa ushindani kazi bado ushindi huu ni ishara nyingine ya kufanya juhudi ili kujiweka kwenye ushindani mchezo ujao.”
Akizungumzia tuzo alisema alichokifanya ni sehemu ya kuipambania timu huku akiwapongeza wachezaji wenzake kwa kucheza kwa kuelewana na kukumbushana majukumu akiweka wazi kuwa wanakazi nyingine ngumu kufikia mafanikio baada ya kukamilisha hatua ya kwanza.
Ramandimbozwa aliibuka shujaa baada ya kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 licha ya wapinzani kwao kufika mara kwa mara langoni mwao alisimama imara.