Vigogo Ulaya, Zelensky uso kwa uso na Trump Jumatatu

Dar es Salaam. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema anapanga kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump mjini Washington kesho Jumatatu baada ya mkutano wa kiongozi huyo wa Marekani na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin huko Alaska.

Hata hivyo jana Zelensky alifanya mazungumzo ya muda mrefu na Trump baada ya kiongozi huyo wa Marekani kukutana na Putin huko Alaska.

Baada ya mazungumzo hayo na Trump, Zelensky pia alifanya mazungumzo na viongozi wengine wa Ulaya kwa njia ya simu.

Alimshukuru Trump kwa mwaliko wa kukutana naye ana kwa ana mjini Washington kesho Jumatatu na kuongeza kuwa watajadili masuala yote ya kukomesha mauaji na vita.

Katika mkutano huo, Rais Zelensky amesisitiza umuhimu wa kuyahusisha mataifa ya Ulaya katika mazungumzo hayo ya amani.

Amesema ni muhimu kwa mataifa hayo kuhusika katika kila hatua ili kuhakikisha kuwepo kwa dhamana za usalama pamoja na Marekani.

Viongozi kadhaa wa nchi za Ulaya wamealikwa kuhudhuria mkutano huo katika Ikulu ya White House.

Taarifa hiyo imetolewa Jumamosi na New York Times, ikinukuu maofisa wawili waandamizi wa Ulaya. Mkutano huo unafuatia kikao cha kilele kati ya Trump na Rais wa Russia, Vladimir Putin kilichofanyika Alaska Ijumaa, ambacho Washington ilisema kilileta ‘maendeleo makubwa’ lakini hakikuzaa makubaliano ya kumaliza mzozo wa Ukraine.

Viongozi  wa Ulaya watafanya mashauriano leo Jumapili mchana kuhusu ziara ijayo ya Rais wa Ukraine mjini Washington. Kwa mujibu wa DW.

Muungano wa Wanaotaka (Coalition of the Willing) utafanya mkutano kwa njia ya video, kwa mujibu wa Ikulu ya Élysée mjini Paris, ikitaja muungano wa takriban nchi 30 zinazoiunga mkono Ukraine unaoongozwa na Uingereza na Ufaransa.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ataongoza mkutano huo pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz.

Mkutano wa Trump, Putin Alaska

Marais Trump na Putin baada ya kumaliza mazungumzo ya saa tatu pamoja na wasaidizi wao, walitoa maneno ya kirafiki lakini hawakujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari jambo lisilo la kawaida kwa rais wa Marekani.

“Hatujafika huko bado, lakini tumepiga hatua. Hakuna makubaliano hadi pale makubaliano yatakapofikiwa,” alisema Trump.

Alitaja mkutano huo kuwa wenye tija kubwa sana na masuala mengi wamekubaliana, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

“Yamebaki machache tu, mengine si ya muhimu sana, lakini moja linaonekana kuwa la muhimu zaidi,” alisema Trump bila kufafanua.

Rais Putin naye alizungumza kwa ujumla kuhusu ushirikiano katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliodumu kwa dakika 12 tu.

“Tunatumaini kwamba uelewano tulioufikia… utafungua njia ya amani nchini Ukraine,” alisema Putin.

Trump alipendekeza mkutano wa pili, na Putin akatabasamu na kusema kwa Kiingereza; “Mara ijayo Moscow.”