KOCHA wa Burkina Faso, Issa Balbone amesema hawana wa kumlaumu kupoteza mechi ya mwisho ya kundi dhidi ya Madagascar kwa vile timu hiyo ilikuwa na kila sababu ya kushinda kutokana na nafasi nyingi za kufunga walizopata, lakini umakini mdogo wa wachezaji ndani ya 18 uliwaangusha.
Burkina Faso iliyoanga michuano hiyo kwa kukusanya pointi tatu tu kupitia mechi nne, ilikumbana na kipigo cha 2-1 juzi usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kuziacha Tanzania iliyomaliza kinara wa Kundi B na Madagascar zikisonga mbele kucheza robo fainali.
Kocha Balbone, alisema licha ya timu hiyo kupoteza mchezo dhidi ya Madagascar wachezaji walionyesha kiwango kizuri na ushindani na makosa madogo waliyoyafanya yamewagharimu kwa vile walishindwa kutumia nafasi walizozipata.
“Tumeaga mashindano hayakuwa malengo yetu nakiri kuwa kuzidiwa mbinu na wapinzani wetu pamoja na kushindwana kutumia nafasi ndio vitu vimetuangusha pamoja na kuchelewa kuwasiri kwa ajili ya kuanza michuano,” alisema Balbone na kuongeza;
“Leo timu yangu imecheza vizuri ilikuwa inakaa kwenye nafasi na kucheza kwa kasi lakini bahati haikuwa upande wetu.” “Nimeridhishwa na upambanaji wa wachezaji wangu licha ya kukosa matokeo nafikiri ni sehemu ya mchezo ambao una matokeo matatu, tulianza vibaya na uchovu kidogo lakini angalau tulianza kuzoea.”