Tanzania, China kushirikiana kuhifadhi historia, utamaduni

Dar es Salaam. Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa China katika kulinda utamaduni na kuhifadhi kumbukumbu za historia kwa manufaa ya vizazi vijavyo katika mataifa hayo.

Rai hiyo ilitolewa jana, Agosti 16, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, wakati wa maonyesho ya picha za kihistoria yenye lengo la kukumbuka historia, kuenzi mashujaa waliopoteza maisha, na kujenga mustakabali bora.

Mwaka huu, China inaadhimisha miaka 80 ya ushindi wa vita vya ukombozi wa watu wa China dhidi ya uvamizi wa Wajapani, vita dhidi ya ufashisti na kurejeshwa kwa kisiwa cha Taiwan chini ya umiliki wa China.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk Pindi amesema maonyesho hayo yanaukumbusha umma namna mashujaa walivyojitoa kwa kuthamini amani inayofurahiwa sasa.

“Ushirikiano na maelewano kati ya Mwalimu Julius Nyerere na ndugu yake wa China, Mwenyekiti Mao Ze Dong, ulichochea amani kwa sababu walihubiri amani na ushirikiano. Hata leo, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka msisitizo kwenye suala la amani, ushirikiano na maridhiano,” amesema Dk Pindi.

Ameongeza kuwa miaka ya 1970, China na Tanzania zilianza kubadilishana tamaduni, ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano uliokuwepo katika maeneo mengine kama vile miundombinu, elimu, afya na kilimo.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema Agosti 15, 1945, Japan ilitangaza kujisalimisha bila masharti, tukio kubwa lililowakilisha ushindi wa vita ya ukombozi wa watu wa China dhidi ya uvamizi wa Wajapani na vita vya dunia dhidi ya ufasisti.

“Vita vya dunia dhidi ya ufasisti vilikuwa na ukubwa usio na kifani katika historia ya binadamu, vikihusisha zaidi ya nchi na maeneo 80 na watu wapatao bilioni 2. Nchi na watu waliopenda amani na haki walinyanyuka kupigana na kujenga umoja wa dunia nzima dhidi ya ufashisti,” amesema.

Amesema kupitia miaka 14 ya mapambano magumu na yenye kumwaga damu, na kwa sadaka kubwa ya zaidi ya askari na raia wa China milioni 35 waliopoteza maisha au kujeruhiwa, wananchi wa China walisimama imara katika uwanja mkuu wa vita vya Mashariki mwa dunia dhidi ya ufasisti, vita ambavyo vilianza mapema na kudumu muda mrefu zaidi na hatimaye wakapata ushindi mkubwa dhidi ya uvamizi wa Kijapani.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga, amesema maonyesho hayo ni sehemu muhimu katika ushirikiano wa Tanzania na China na wanaahidi kuendelea kushirikiana katika kuhifadhi kumbukumbu muhimu za ushirikiano baina yao.

“Makumbusho ya Taifa tumekuwa tukishirikiana na balozi mbalimbali zilizopo hapa nchini. Tunafurahi kushirikiana na China katika maonyesho haya muhimu kwani yanatukumbusha historia ya China, jinsi ilivyopambana kulinda amani na mustakabali wake,” amesema Dk Lwoga.