KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua jijini Cairo, Misri, lakini unaambiwa tangu juzi mabosi wa klabu hiyo wamekuwa katika hesabu kubwa za mwisho ya kushusha mashine nyingine mpya ili kuimarisha kikosi hicho.
Inadaiwa kuwa, mabosi wa Simba walivutiwa waya na Kocha Fadlu Davids akitaka aongezee mashine nyingine mpya ya kucheka na nyavu na fasta kupitia bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ alionyesha umwamba kwa kujitosa ili kuhakikisha mashine hiyo inatua kabla ya kufungwa kwa usajili.
Staa aliyemfanya Mo Dewji kutunishiana misuli na Waarabu ni Mtanzania anayekipiga Wydad Casablanca ya Morocco wanayetaka kumrudisha nchini, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyeondoka Tanzania akiwa amefunga mabao sita katika Ligi Kuu, licha ya kutumika kwa muda mfupi kutokana na kusumbuliwa na majeraha wakati akiitumikia Fountain Gate.
Inadaiwa kuwa, kocha Fadlu bado haridhishwi na nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, lakini hapohapo akiwa na maumivu ya kumkosa kiungo chaguo lake namba moja Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyeamua kubaki klabuni kwake Azam FC.
Simu moja tu ya Fadlu kwa MO imemtingisha tajiri huyo na kuwavamia Wydad Casablanca ya Morocco akimtaka Mwalimu iwe kwa kuuziwa mazima hatua ambayo Waarabu hao wameigomea.
Hatua ya pili ambayo Wydad hadi jana ilikuwa inaelekea kukubali ni kumtoa kwa mkopo, lakini kwa masharti mawili ambayo bado MO amekubaliana nayo.
Masharti hayo mawili, ingawa yana gharama kubwa lakini MO amekubaliana nayo ni pamoja na kuulipia mkopo huo kiasi cha Dola 100,000 (sawa na TSh 260 Milioni) ambazo zinatakiwa kulipwa haraka kwa Wydad.
Sharti la pili ambalo Wydad imeipa Simba ni kwamba, Wekundu hao watakuwa kumlipa Mwalimu mshahara wake wote pasipo Waarabu hao kuweka chochote na tajiri akasema sawa.
Mwanaspoti linafahamu kuwa, pande hizo mbili zilikuwa zinamalizia kubadilishana mikataba hiyo kuanzia Ijumaa ili Mwalimu awahi dirisha la uhamisho.
Hesabu za ujio wa Mwalimu zinaweza kuchochea mshambuliaji Leonel Ateba kutupwa nje ya kikosi hicho ch Msimbazi, baada ya wekundu hao kuwa na hesabu za kupunguza wachezaji wa kigeni ili kutimiza idadi kamili ya wachezaji 12 inayohitajika kikanuni.
Simba ilikuwa inataka kumfanya Mwalimu kuwa jina kubwa la usajili wao wa msimu huu baada ya kumkosa Fei Toto ambaye alitakiwa kubeba mauzo ya jezi za wekundu hao kwenye tamasha la Simba Day.
“Tulitaka kufanya siri, lakini naona imeshindikana, tulitaka kumtambulisha kama sapraizi Gomes ila mchakato wake ulilazimisha hadi klabu yake ya zamani ujue na hapo ndipo siri ilipovuja,” alisema bosi huyo wa Simba.
Kabla ya kuuzwa Wydad akiwa anaitumikia Fountain Gate kwa mkopo akitokea Singida Black Stars ambaye ndiyo iliyomuuza kwa Wamorocco na kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki Fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025 zilizofanyika Marekani.
Mwalimu alikuwa mshambuliaji tishio akiongoza kwa ufungaji ambapo mpaka anaondoka alikuwa amefunga mabao Sita na asisti tatu akiwa na na tuzo saba zikiwemo sita za mchezaji Bora wa mechi na Moja ya mchezaji Bora wa mwezi.