Daruweshi achekelea kambi ya visiwani

MSHAMBULIAJI wa KMC, Daruwesh Saliboko ameshindwa kujizuia na kufunguka namna alivyofurahia kambi ya maandalizi ya msimu mpya kwa timu hiyo iliyokuwa visiwani Zanzibar, anaamini imewajenga vyema kwa kuanza msimu mpya kivingine.

KMC ilikuwa imejichimbia Zanzibar tangu wiki iliyopita kabla ya jana kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa FA wa visiwani hivyo, KMKM na leo ikiwa njiani kurejea ili kuendelea kujifua zaidi jijini Dar es Salaam chini ya kocha Marcio Maximo kutoka Brazili.

Saliboko aliliambia Mwanaspoti kwa muda waliokuwa kambini Zanzibar imewasaidia kupata utulivu wa akili na kufanya mazoezi yanayowaandaa kulingana na ugumu wa Ligi Kuu utakavyokuwa kwa msimu ujao.

“Kadri muda unavyokwenda ndivyo Ligi Kuu inavyokuwa ngumu, maandalizi ya msimu ndiyo kila kitu kwa maana tukiyafanya ipasavyo kwa kuzingatia kile wanachokitaka makocha basi tutakuwa na wakati mzuri wakati wa mechi,” alisema Saliboko na kuongeza;

“Mfano msimu uliyopita ushindani ulikuwa mkali kwa wazawa kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemaliza kama kinara wa asisti 13 kwa wageni katika nafasi ninayocheza  nilipenda aina ya uchezaji wa Steven Mukwala wa Simba aliyemaliza na mabao 13 , hiyo ni tafsiri ya ligi ijayo haitakuwa rahisi.”

Nyota huyo wa zamani wa Lipuli Iringa na Polisi Tanzania, alikiri kwa upande wake msimu uliyopita haukuwa mzuri na alimaliza na mabao mawili na asisti mbili na FA alimaliza na mabao mawili na asisti moja, hivyo msimu ujao anatamani kurejea kivingine.

“Nilisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale, hivyo sikuwa na wakati mzuri wa kucheza mechi nyingi ndiyo maana napambana zaidi katika mazoezi tunayoyafanya ili Ligi Kuu ijayo niwe miongoni wa wafungaji wenye mabao mengi,” alisema Saliboko aliyefunga mabao 12 msimu wa 2019/20 akiwa Lipuli.