Maandalizi ya CAF, KMKM yabeba kocha mpya

WAWAKILISHI wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika, KMKM imemnyakua kocha mpya kutoka Dar ili kujiweka tayari kwa pambano dhidi ya As Port ya Djibouti.

Mabingwa hao wa Kombe la ZFF, imemuongeza kikosini kocha wa kituo cha JK Park cha jijini Dar es Salaam, Hababuu Ali kulisaidia benchi la ufundi la timu hiyo.

KMKM imepata nafasi ya uwakilishi huo baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho (ZFF) ambao wamefanya uamuzi wa kuongeza nguvu baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ame Msimu kutokukidhi vigezo vya CAF.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msimu alisema ni kweli wameongeza nguvu benchi la ufundi lengo ni kuona timu hiyo yenye rekodi ya kushiriki michuano ya kimataifa mara nyingi inafanya vizuri mwaka huu.

“Lakini kitu kingine ni kwamba mimi sina leseni inayotambulika na CAF, ndio maana uongozi umefanya juhudi ya kuongeza nguvu kwa kumchukua kocha Ali ambaye amekidhi vigezo,” amesema Msimu na kuongeza;

“Mbali na vigezo hivyo pia ni kocha mwenye uwezo mkubwa wa mbinu nafikiri atanisaidia sana kuhakikisha timu hii inafanya vizuri mwaka huu, hatutaki kuendeleza rekodi ya kuishia hatua za awali.”

Akizungumzia maandalizi na usajili amesema maandalizi yanakwenda vizuri na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri ya ushindani na amefanya usajili kulingana na mahitaji.

“Timu ipo vizuri na imerudishwa mazoezini mapema kwa lengo la kujiweka katika mazingira mazuri ya ushindani, nawashukuru viongozi wamefanya usajili kulingana na mahitaji kilichobaki ni kuona tunafanya kitu kizuri.”

KMKM katika michuano ya kimataifa inatarajia kuanzia ugenini kati ya Septemba 19 ikiikabili AS Port kabla ya kurudiana Septemba 26.

Mshindi wa jumla wa  mechi hizo za raundi ya kwanza atacheza na mshindi kati ya Azam Fc na Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini.