Pogba aichomolea Tabora United, kuendelea kukipiga Mlandege

LICHA ya kusaini mkataba wa miaka miwili ili aitumikie Tabora United, kiungo mshambuliaji wa Mlandege, Juma Kidawa ‘Pogba’ ameendelea kuitumikia timu hiyo iliyopo kambini.

Ipo hivi. Pogba aliyekuwa akihusishwa na Simba kabla ya mpango kufa baada ya Wekundu hao kumnasa Daud Semfuko kutoka Coastal Union, aliibukia  Tabora na kufanikiwa kusaini mkataba kabisa.

Hata hivyo, mapema leo nyota hiyo akiwa mazoezi ya Mlandege ameliambia Mwanaspoti, ni kweli amesaini mkataba Tabora  baada ya makubaliano ya kila kitu, lakini hadi sasa haelewi nini kinaendelea kwani bado hajaingiziwa fedha.

“Kuhusu Simba nilifahamu, kuna ofa lakini sijawahi kuzungumza viongozi hilo niliwaachia wasimamizi wangu ambao hawakunirudia, ndipo ilipokuja ofa ya Tabora United ambayo kila kitu kilikamilika na nimesaini mkataba,” amesema Pogba anayefaninishwa kiuchezaji na kiungo Mfaransa Paul Pogba aliyepo Monaco kwa sasa.

“Licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili hadi muda huu sijaingiziwa fedha yoyote, ndio maana unaniona nipo hapa Mlandege naendelea na mazoezi kwa ajili ya msimu mpya na michuano ya kimataifa.”

Pogba alisema yeye ni mchezaji ana uwezo wa kucheza popote, lakini anazingatia maslahi,  hivyo ataendelea kupambana akiwa Mlandege muda ukifika wa kuondoka atafanya hivyo.

“Nilitamani kutoka kwenda kujaribu maisha Tanzania Bara, lakini mpango haujaenda sawa tofauti na matarajio yangu. Lakini hilo halinifanyi nikashindwa kuendelea kupambana,” amesema Pogba.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla timu hiyo itakayoshiriki   Ligi ya Mabingwa Afrika amesema yanaenda vizuri na wana matarajio makubwa kufanya vizuri.