Morogoro. Katika Kijiji cha Ngerengere, wilayani Morogoro, anaishi Ally Mikola (76), kwa zaidi ya miaka 20, alikuwa mfanyabiashara wa mkaa, akiupeleka Dar es Salaam na maeneo mengine kwa ajili ya kujipatia kipato.
Siku hizi, badala ya kuendelea na biashara hiyo, anahamasisha wananchi kutumia nishati safi na mkaa mbadala ili kulinda misitu na afya ya jamii.
“Nilianza biashara ya mkaa mwaka 2005. Nilipata faida na niliweza kuendesha familia yangu. Lakini baadaye niliona athari zake kama misitu inapotea, mazingira yanaharibika na moshi wa mkaa unaleta matatizo ya kiafya” anasema Mikola ambaye pia ni balozi wa nyumba kumi kwenye mtaa wake.
“Sasa hivi natumia mkaa mbadala na ninawahamasisha wenzangu tufanye hivyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo”.
Anasema mkaa huo wanatengeneza kwa kutumia mabaki ya vyakula, mbao na vyanzo vingine kama mabua, hivyo si tu wanasafisha na kulinda mazingira lakini wanabadilisha bidhaa ambazo pengine zingekuwa kero kuwa fursa muhimu ya kiuchumi.
Mikola anasema hakuanza hivi hivi ila baada ya kupata elimu na kuona uhalisia wa mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira.
Mafunzo ya elimu na uhamasishaji alipewa na Kikundi cha Vijana wa Ngerengere General Supplies, kinachoongozwa na Yustino Chiwaya.
Mafunzo hayo walipata mwaka 2024 kupitia mradi wa Uwezeshaji wa Jamii katika Usimamizi Endelevu wa Misitu na Nishati Mbadala (Usemi).
Kwa kutumia mabaki ya kilimo kama maganda ya miwa, vifuu vya nazi, mabunzi ya mahindi na vumbi la mbao, kikundi hiki huzalisha mkaa mbadala na kuwafundisha wananchi namna unavyoweza kuchukua nafasi ya mkaa wa miti.
Ngerengere, kama maeneo mengine ya Morogoro, imeathiriwa na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wamekuwa wakitegemea mkaa kutoka ukanda huu kutokana na misitu yake ya awali kuwa mikubwa na yenye rutuba.
Pia, hali imebadilika, misitu imepungua kwa kasi na athari za kimazingira zimeanza kuonekana wazi.
Chiwaya anasema, kikundi chao huzalisha zaidi ya tani moja ya mkaa mbadala kwa siku kwa kutumia mashine maalumu walizopatiwa.
Hata hivyo, anakiri changamoto bado ni kubwa.
“Tunahangaika na uelewa mdogo wa jamii, miundombinu duni na ukosefu wa soko la uhakika. Haya yote yanakwamisha kasi ya kueneza mkaa huu mbadala,” anasema.
Kuhusu mchakato wa kuzalisha mkaa huo, anasema: “Tunakusanya malighafi, tunachoma kwenye tanuli, kisha tunayasaga na kuchanganya na unga wa mbao na uji wa muhogo ili kushikamanisha. Baada ya kukausha kwa siku tatu, mkaa unakuwa tayari kutumika.”
Kiongozi mwingine wa Kikundi cha Ngerengere General Supplies, Maimuna Lupesa anasema tatizo ni ukosefu wa usimamizi madhubuti wa sheria.
“Watu hukata miti ovyo kwa sababu hakuna ufuatiliaji wa karibu. Sheria zipo, lakini utekelezaji wake bado ni dhaifu,” anasema.
Licha ya changamoto hizo, jitihada za kikundi hicho zimeanza kuzaa matunda. Baadhi ya familia tayari zimeanza kutumia mkaa mbadala na kushuhudia faida zake.
Hidaya Shabani, mkazi wa kijiji hicho, anasema mkaa wa miti ulikuwa ukimsababishia matatizo ya macho.
“Nilikuwa nikipika macho yananiwasha sana, lakini tangu nianze kutumia mkaa mbadala hali hiyo haipo tena. Nawaomba wanawake wenzangu, hasa sisi tunaoathirika zaidi na moshi jikoni, tuhamie kwenye nishati safi,” anashauri.
Akizungumzia mafanikio ya kikundi hicho, Mikola anasema: “Sasa hivi ninaposhuhudia watu wakiokoa misitu na afya zao, najiona mwenye furaha zaidi kuliko wakati nilipokuwa nikiendesha biashara ya mkaa wa miti.”
Ushirikiano wa Serikali na wadau
Dalali Venge kutoka Usemi anasema kazi ya kikundi hicho ni mfano wa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi wa 2024–2034.
Anasema mkakati huo unaweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Rosemary Semiono anatambua jitihada za wananchi hao akisema halmashauri imekuwa ikiendesha semina na warsha vijijini ili kuelimisha wananchi kuhusu mbinu mbadala, ikiwamo matumizi ya biogesi.
“Tumeona wananchi wakipewa elimu sahihi, hawahitaji kushinikizwa. Asilimia 75 ya wananchi wetu ni wakulima na wafugaji. Wana mabaki ya mazao na kinyesi cha mifugo ambacho ni rahisi kutumika kuzalisha biogesi majumbani,” anasema Semiono.
Anasisitiza kuwa wanaendelea kushirikiana na wataalamu mbalimbali ili kufikisha elimu shuleni na kwenye jamii kwa upana zaidi.
“Kila kaya inaweza kutumia rasilimali zilizopo karibu yake kuandaa nishati safi. Tukifanikiwa, tutaokoa misitu na kuboresha afya za wananchi,” anasema.
Chiwaya anasema ili jitihada kama hizi zifanikishwe kwa kiwango kikubwa zaidi, kunahitajika ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii.
Anafafanua kuwa sheria za kudhibiti ukataji miti lazima zitekelezwe kikamilifu, vikundi vya kijamii vinavyohamasisha nishati mbadala vipatiwe msaada wa kifedha na vifaa, na soko la nishati safi liwekwe katika mfumo thabiti wa upatikanaji.
Mikola anasema maisha yamekuwa funzo la thamani kwake kutokana mfanyabiashara wa mkaa hadi balozi wa nishati safi.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.