KOCHA wa DR Congo, Otis Ngoma ameonyesha masikitiko yake baada ya timu yake kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024, licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika baadhi ya vipindi vya mechi ya mwisho ya kundi A dhidi ya Morocco.
DR Congo ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa CHAN imefungashiwa virago vyake huko Kenya baada ya kushindwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kufuatia kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Morocco.
Ngoma alisema kutokuwa makini kuligharimu kwa sababu Morocco walitumia udhaifu huo kupata matokeo.
Alisisitiza makosa madogo yalileta tofauti kubwa baina ya timu hizo mbili, na ndiyo sababu kwa DR Congo kuishia hatua ya makundi.
“Kusema kweli tulishindwa kutumia nafasi tulizozipata na mwisho wa siku tukalipia. Pia, niliiona timu yangu ikikosa maelewano katika idara zote, jambo lililowapa Morocco nafasi ya kutuadhibu,” alisema na kuongeza;
“Ni huzuni kubwa kuondoka hatua ya makundi, lakini tunapaswa kurudi mezani, kuchambua makosa na kurejea tukiwa bora zaidi. Hongera kwa Morocco kwa kusonga mbele, walicheza vizuri.”
DR Congo iliingia katika michuano hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kutwaa ubingwa mara mbili, hali iliyoongeza matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wao. Hata hivyo, historia hiyo haikutosha kuwabeba.