Dar es Salaam. Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umemchagua Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina kuwa Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo, huku Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akichaguliwa kuwa mwenyekiti atakayefuata.
Mkutano huo umemchagua Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama huku Mfalme Mswati III wa Eswatini akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo atakayefuata.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi ulifanyika jana Agosti 17, 2025 jijini Antananarivo, Madagascar ukihudhuriwa na viongozi kutoka mataifa 16 wanachama ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliwakilishwa na makamu wake, Dk Philip Mpango.
Pamoja na mambo mengine mkutano huo ulipokea ripoti kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Rais Samia iliyowasilishwa na Dk Mpango na kumpongeza kwa uongozi wake bora na kujitolea kwake katika kuendeleza amani na usalama katika ukanda huo, wakati wa kipindi chake cha uongozi.
“Mkutano ulisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kuendeleza amani, usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ukakaribisha juhudi za pamoja za upatanishi zinazotekelezwa na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na mchakato unaounganisha mchakato wa amani wa Luanda na wa Nairobi.
“Mkutano huo umetambua haja ya dharura ya ulinganifu na uratibu kati ya michakato inayoongozwa na Afrika na juhudi nyingine, zikiwemo Makubaliano ya Washington ya mwaka 2025 na Azimio la Doha la mwaka 2025,” inasomeka sehemu ya taarifa ya pamoja la SADC.
Aidha, taarifa hiyo inabainisha kwamba mkutano uliipongeza Lesotho kwa kupitishwa na kuanza kutekelezwa kwa marekebisho ya 10 ya katiba ya Lesotho, hatua muhimu katika kuendeleza na kukamilisha mchakato wa mageuzi ya kitaifa nchini humo.
Katika mkutano huo, viongozi hao waliipongeza Tanzania kwa kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Nishati Afrika wa Mission 300 uliofanyika Januari 2025 jijini Dar es Salaam na ukaielekeza sekretarieti kushirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na wadau wengine wa maendeleo ili kusaidia nchi wanachama katika kuandaa mikataba ya kitaifa ya nishati ifikapo mwishoni mwa 2025.
Pia, ulihimiza nchi wanachama kuendeleza ushiriki kamili na wenye tija wa wanawake katika michakato ya kisiasa na ya kufanya uamuzi, kuimarisha mifumo ya kitaifa ya ukusanyaji wa takwimu kwa uratibu pamoja na tafiti za mara kwa mara kuhusu Ukatili wa Kijinsia (GBV), na kuongeza msaada na ufadhili kwa mipango inayoshughulikia chanzo kikuu cha ukatili huo.
Wakati huohuo, mkutano wa wakuu wa nchi ulitoa rambirambi za dhati kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Namibia, Dk Samuel Nujoma, Rais wa sita wa Zambia, Dk Edgar Lungu, Makamu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, David Mabuza, Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Eswatini, Seneta Constance Simelane na Waziri Mkuu wa zamani wa Eswatini, Mtemi Mabandla Dlamini.